Kikao cha kwanza cha mazungumzo ya maridhiano kati ya serikali na mrengo wa Upinzani kimeanza katika ukumbi wa Bomas jijini Nairobi.
Kikao hicho cha wanakamati 10 walioteuliwa na muungano wa Azimio na Kenya Kwanza kinaongozwa na Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah na Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka.
Kwenye hotuba yake ya ufunguzi kabla ya mazungumzo kuanza rasmi, Kiongozi wa Ujumbe wa AZIMIO kwenye mazungumzo hayo Kalonzo Musyoka ameweka bayana kuwa mazungumzo hayo hayatajadili masuala binafsi ya viongozi wala ugawanyaji mamlaka.
“Hatutajadiliana kwa namna yoyote mambo ya kugawana mamlaka. Pia hatutaweka maslahi ya kiongozi wetu yeyote badala ya Wakenya,” akasema Kalonzo.
Kalonzo aidha amebaini kuwa wanatarajia mazungumzo hayo yatazingatia hadhi ya walioshiriki sawia na kuzingatia sheria na katiba ya nchi.
Gavana wa Embu Cecil Mbarire aliongoza Ujumbe wa Serikali Kenya Kwanza akimwakilisha Kiongozi wa Wengi Bungeni Kimani Ichung’wah, alisema kuwa wamekuja kwa nia njema na kuhakikishia Azimio kuwa watashirikiana kwa kila hatua ya mazungumzo hayo na kuweka maslahi ya Wakenya mbele.
“Tunataka kuwaahidi Timu ya Azimio kuwa tuko hapa kujadilia masuala tutakayoyaweka na tutaendelea kushauriana hapa ndani na walio nje ya ili kuja na suluhu la kudumu kwa changamoto zinazowakabili Wakenya, na tunaamini tutapata suluhu ili kuendeleza nchini mbele na kudumisha amani,” alisema Mbarire.
Upande wa Kenya Kwanza aidha ulkuwa na Kiongozi wa Wengi katika bunge la Seneti Aaron Cheruiyot, Mbunge wa EALA Hassan Sarai na Catherine Wambilianga.
Muungano wa AZIMIO nao ulikuwa na Kiongozi wa Wachache Bunge la Kitaifa Opiyo Wandayi, Kiongozi wa chama cha DAP-K Eugene Wamalawa, Seneta wa Nyamira Okong’o Omogeni na Amina Mnyazi, Mbunge wa Malindi.
Baada ya hotuba za ufunguzi za Kalonzo na Mbarire wanahabari walitakiwa kuondoka katika ukumbi huo ili mazungumzo kuanza rasmi.
BY EDITORIAL DESK