HabariLifestyleNews

Viongozi na Mashirika Wakashifu semi za Inspekta Jenerali kuhusu Waliofariki Maandamano

Mashirika ya kijamii Pwani yamekashifu kauli ya Inspekta Jenerali wa Polisi Japhet Koome kudai mrengo wa upinzani uliwahadaa Wakenya kwa kutumia picha zisizo za kweli za miili waliofariki kwengineko na kulimbikizia lawama kwa maafisa wa usalama nchini.

Afisa wa Masuala ya Dharura kutoka shirika la MUHURI Francis Auma amesema kauli hiyo imeonyesha kuwa Koome amejiingiza kwenye mambo ya kisiasa jambo ambalo amelitaja kuwa kinyume cha majukumu yake katika serikali.

“Inaonyesha kuwa amekuwa mwanasiasa sasa, anafurahia wananchi kuuawa. Hatutaogopa tutamfuatilia na hata kumshtaki kwa kauli hizo zisizojali,” akasema Auma.

Ni Kauli iliyoungwa mkono na Bradley Ouna Mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu kutoka shirika la Concern Citizen of Kenya akisema tamko hilo limeonyesha ni mtu asiye na hisia kwa waliojeruhiwa na hata kupoteza maisha yao kutokana utumizi wa nguvu kupita kiasi.

Naye Mwenyekiti msaidizi katika Baraza la Maimamu na Wahubiri nchini, CIPK kaunti ya Mombasa Sheikh Khamis Aula amekosoa matamshi ya Inspekta Jenerali wa polisi Japhet Koome akisema kuwa kiongozi huyo hakufaa kuyatoa matamshi hayo hadharani, akiwataka viongozi kuchuja na kupima kauli zao wanapokuwa hadharani akisema kuwa huenda baadhi ya semi zikachochea chuki na hisia kali miongoni mwa Wakenya.

“Kuna mambo hayapaswi kusemwa hadharani na viongozi wakubwa kwenye jamii kama yeye. Yanazua hofu na kuleta uhasama ni vyema viongozi wakachuja kauli zao,” alisema Sheikh Aula.

Itakumbukwa mnamo siku ya Jumanne, Agosti 8 Inspekta Jenerali wa Polisi Japheti Koome akiwa huko Nyeri alisema kuwa Upinzani na mashirika walikodisha umia picha za wafu waliofariki katika matukio mengine kueneza propaganda kwa kuharibu sifa ya idara ya polisi na kuilimbikizia lawama.

“Walienda mochari kukodisha miili kisha kuita wanahabari na kuwaambia kuwa watu hawa waliuawa na polisi, kivipi viongozi hawa wanafikiri kuwa sheria inaweza kudhaniwa hivyo? Nataka kuchukua fursa hii kuwaambia wakenya wenzangu kuwa kama Huduma ya Kitaifa ya Polisi tuna jukumu la kulinda maisha na mali, na tutafanya tuwezalo kulinda Amani na usalama wa taifa” Alisema Koome.

Itakumbukwa kuwa Chama cha Wanasheria nchini LSK kwa ushirikiano na shirika la Kimataifa la kutetea haki za Kibinadamu Amnesty International katika ripoti yao ilibaini kuwa watu 107 walijeruhiwa kwenye mandamano hayo, na 47 kati yao walikuwa na majeraha ya risasi.

Aidha Miiongoni mwa walioaga dunia ama kujeruhiwa kuna kadhaa ambao hawakuwa katika mazingira ya maandamano.