HabariLifestyleNews

Kaunti ya Mombasa Kuanzisha Masomo ya Ziada kwa Wanafunzi Msimu wa Likizo

Serikali ya kaunti ya Mombasa kupitia wizara ya elimu inalenga kuanzisha masomo ya ziada kwa wanafunzi wa shule za upili wakati huu wa likizo ya muhula wa pili. 

Akizungumza katika Hafla ya kuwatuza wanafunzi waliofanya vyema katika shule mbali mbali katika Jumatano Agosti 9, siku ambayo pia ni ya kusherehekea Siku ya Elimu kaunti ya Mombasa,  Gavana wa Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir alisema mpango huo utasaidia pakubwa kuinua kiwango cha elimu na hatua moja wapo ya kuandikisha matoke bora kwa wanafunzi.

“Huu mpango utakuwa wenye kutekelezwa na shule zote katika kaunti ya Mombasa,nilikuwa nimeomba iweze kufanywa hadi kuanzia 1,2,3 na 4,lakini washikadau wamejaribu wamenishawishi ya kuwa sasa hivi kwa sababu ni program kubwa,likizo hii itatekelezwa kwa wanafunzi wa vidato vya 3 na 4 kwanza.” Alisema Nassir.

Wakati huo huo gavana Nassir alisema analenga kufufua shule zote za chekechea kaunti ya Mombasa zilizokuwa zimesimama kutokana na ukosefu wa fedha huku akipania kuajiri walimu wa chekechea zaidi.

“Nimetoa amri kabla ya hatujaanza kufikiria kujenga ECDE nyingine zile ambazo zilikuwa zimesimama kwa sababu moja au nyingine zimalize kujengwa na ni matumaini yetu kuwa zitakamilika mwishoni mwa mwaka huu na kuanza kufanya kazi mwaka ujao.” Alikariri Gavana.

Katika hafla hiyo ililiyohudhuriwa na wadau mbalimbali wa elimu Mwenyekiti wa Muungano wa wazazi kaunti ya Mombasa Robert Mukendi amehimiza wazazi kuwajibika katika shughuli za kieleimu za watoto wao kwa kuwafuatilia shuleni.

“Wazazi lazima tushiriki katika ukuaji na elimu ya watoto ili tuweze kuvuna matunda mema kutoka kwa hawa watoto.Hauwezi ukatarajia kuvuna matunda na hujashiriki katika ukuaji wa mtoto, haujampalilia ,haujampa kile kinachohitajika.”Alisisitiza Mukendi.

NA MJOMBA RASHID