HabariNews

Makenzie aitaka Serikali Imuue na Kutupa Mwili wake Mto Yala

Kwa mara nyingine tena mhubiri mwenye utata Paul Makenzie ameibua kizaazaa katika Mahakama ya Shanzu alikofika kusikiliza kesi.

Makenzie na wenzake 29 ambao wamefikishwa mahakamani kujua hatima yao ya iwapo wataendelea kuzuiliwa kwa siku 47 au la, ameendelea kulalamikia kunyimwa na kukiukwa kwa haki zake na washukiwa wenzake.

Mbele ya mahakama hiyo Makenzie Amewaongoza washukiwa wengine kuimba nyimbo za ‘haki yetu’ huku akipiga kelele na kulia kwa sauti akiwalaumu maafisa wa polisi kwa kumdhulumu kwenye seli.

Vilevile amedai kuwa hajakuwa akila kwa siku mbili wala kuoga kwani amefungiwa katika chumba maarufu ‘dark room’ huku akidai kunyimwa dhamana akisema kuwa serikali inaendelea kumdhulumu.

Makenzie sasa anaitaka serikali kumwua mara moja na kisha kuurusha mwili wake katika Mto Yala.

Wakati wa kusiklizwa kwa kesi hiyo Alhamisi Agosti 10 Hakimu Mkuu Yusuf Shikanda aliyasoma baadhi ya majina ya waathiriwa.

“24, Julius Katana Kazungu eneo la Ganda, Malindi aliishi Shakahola na watoto wake 2 wote wamepotea, mwengine ni Evans Kulombe Sirya kutoka Kisimani Malindi, ripoti ya uchunguzi ilionyesha kuwa mwanachama wa Good News International church na alikuwa Shakahola na mke wake na watoto 6, Mkewe huyo na watoto wote 6 wamepotea….” Alisema Hakimu Shikanda.

Ikumbukwe kuwa Mackenzie mkewe Rhoda Maweu na washukiwa wengine wanakabiliwa na mashtaka ya mauaji ya zaidi ya watu 400, utekaji nyara na kutoa mafunzo ya itikadi kali ambapo anadaiwa kuwaagiza wafuasi wake kufunga hadi kufa ili kwenda mbinguni kukutana na Yesu.