HabariNews

Vijana Wakumbatie Ubunifu na Kazi za Mikono badala ya Kusubiri Kuajiriwa

Huku taifa likijiandaa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Vijana Ulimwenguni, vijana kaunti ya Mombasa wameusiwa kujihusisha na kazi za mikono badala ya kutegemea ajira ofisini.

Kundi la vijana liitwalo CocoHuru na linalojihusisha na utengenezaji wa vitu tofauti tofauti kutoka kwa taka za plastiki umerai vijana kuwa wabunifu na kuja na mbinu mbali mbali ya kujiajiri kama njia ya kujitafutia mapato.

Wakiongozwa na Javan Mugendi mmoja wa vijana kutoka kundi hilo amesema azma yao ya kutumia taka za plastiki ni kuimarisha usafi mjini Mombasa.

“Ile akili uko nayo, kile kitu unafikiria unaweza kutengeneza kitengeneze onyesha mwenzako kwamba unaweza kutengeneza kitu fulani usitengemee kutengenezewa kazi ama kuangalia kama kuna mtu mbele kunitafutia kazi.” Alisema Javan

Aidha Javana amesema kuna biashara nyingi sana zinaweza kuanzishwa na zikazaa matunda kwa kutegemea kiwango cha elimu mtu na ubunifu wa mtu.

Wakati huo huo Javan amerai viongozi na mashirika mbali mbali ikiwemo Mamlaka ya kudhibiti usafi wa mazingira nchini NEMA kuwaunga mkono katika shughuli zao akisema kwa kufanya hivyo wataimarisha usafi wa mazingira mjini Mombasa.

“Tunahitaji sana NEMA na wale watu wa kushughulikia usafi wa bahari na mashirika mengine, tunaamini kwa kufanya hivi tutaweza kufanikisha usafi wa mazingira na kupunguza taka za plastiki hapa Mombasa.” Alisema Javan

Pia ameongeza kuwa vijana wapo tayari kuhakikisha usafi unaimarishwa Mombasa akisisitiza haja ya kuwepo kwa uungwaji mkono kutoka kwa serikali ya kaunti hiyo.

Haya yanajiri huku taifa likijandaa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Vijana itakayodhimishwa Jumamosi tarehe 12 Agosti, kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ikiwa ni ‘Green Skills for Youth: Towards a Sustainable World.’

Siku hiyo iliasisiwa na Umoja wa Mataifa kuangazia masuala ya tamaduni na masuala ya sheria yanayozunguka vijana na iliadhimishwa kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 2012.

BY EDITORIAL DESK