HabariLifestyleNews

Ripoti: Zaidi ya Miaka 10 ya Ugatuzi, Wakenya wangali Kufurahikia matunda yake ipasavyo

Huku ikiwa ni Miaka 10 ya serikali za ugatuzi ripoti ya utafiti uliofanywa na mashirika mbalimbali imeonyesha kuwa wananchi wengi hawajaridhishwa na utenda kazi wa serikali za kaunti.

Ripoti hiyo iliyoshirikisha Mashirika ya kijamii ya kutoka kaunti 4 ikiwemo Nairobi imetolewa katika hafla ya kutathmini mafanikio ya ugatuzi nchini, saa chache kabla ya kuanza kwa kongamano la Ugatuzi, linaloanza Siku ya Jumanne Agosti 15.

Miaka zaidi ya 10 tangu serikali za ugatuzi kushika usukani nchini matunda ya ugatuzi yangali kufanikishwa kikamilifu, huku changamoto kadha wa kadha zikiwemo uhaba wa fedha na utumizi mbaya wa raslimali zikitajwa kutishia ufanikishaji wa ugatuzi.

Kulingana na Evans Kibet ambaye ni Msemaji wa Mashirika ya kijamii ya kaunti za Uasin Gishu, Nairobi, Ukambani na Mlima Kenya, Serikali za Kaunti zimekuwa zikipokea ufadhili kwa kuchelewa hivyo basi kuathiri utendakazi wa serikali za kaunti.

“Swali Kuu Wakenya wanajiuliza ni je, tumeifanikisha kweli ndoto ya ugatuzi? Moja ya sababu zinafanya bajeti za kaunti kukosa kutekelezwa kikamilifu ni ucheleweshwaji wa fedha za kaunti, ila hatujafumbia macho ufisadi, utumiaji mbaya wa raslimali za kaunti ni kikwazo kwatika kaunti.” Akakasema Kibet.

Sauti ya Pwani imekita kambi mjini Eldoret kaunti ya Uasin Gishu ambako Kongamano hilo litafanyika, na tutakuletea kila tukio kutoka huko, mahojiano ya moja kwa moja na taarifa za kina.