Kamati ya bunge la kitaifa kuhusiana na hazina ya Ustawishaji wa Maeneo Bunge NG-CDF imetaka kipengele cha sheria cha Hazina hiyo kutambulika kwenye katiba ili kuhakikisha wabunge wanafanya majukumu yao bila matatizo yoyote.
Naibu wa mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye ni Mbunge wa Matunga Kassim Tandaza amepinga kuhusu kuondolewa kwa hazina hiyo akisema imechangia maendeeleo mengi katika maeneo ya mashinani.
Tandaza amesisitiza kuwa kamati hiyo inaendeleza kukusanya maoni ya wananchi Kaunti ya Kwale kwenye shule ya msingi ya Vuga kuhusiana na vipengele vyenye utata kwenye hazina ya CDF ambayo vilisababisha korti kuharamisha hazina hiyo.
“Tunakubaliana kwamba kuna mambo mengine ambayo CDF ilikua inafanya na ni mambo ya kaunti kwa mfano mambo ya michezo hasa kwa upande wa shule, kaunti huwa hawashughuliki na michezo ya shule kwa hivyo wazazi wamependekeza iendelee japo kikatiba kuna hilo pingamizi.”alisema Tandaza.
Tandaza ameongeza kuwa wanamatumaini kwamba baada ya kuchukua maoni bunge litaweza kulainisha katiba na sheria ya NGCD kuhakikisha hazitakuwa na mtafaruku wowote.
Kwa upande wake kongozi wa Bodi hiyo Maria Lekoloto amesema bodi hiyo imeanzisha mradi wa ujenzi wa madarasa ya shule ya sekondari msingi JSS pamoja na kufungua bweni ya wasichana kwenye shule ya Vuga iliyogharimu shilingi milioni 3.
“Tunawapa maeneo bunge ambayo yanafanya kazi vizuri kwa mfano sasa tumetoa maeneo bunge 4 na hii ni kuongeza katika miradi yao ambayo wanatekeleza huko chini na.”Amesema Lekoloto.
Itakumbukwa kuwa mwaka jana Mahakama ya Juu iliamua kuwa Hazina ya CDF kuwa kinyume cha sheria na kutaka kubanduliwa.
Kwenye uamuzi wake mnamo Agosti 8 mwaka 2022 Jaji Mkuu Martha Koome alisema kuwa sheria iliyobuni hazina hiyo ya CDF ni kinyume cha katiba na kipengee kilichotengeneza sheria hiyo kilihujumu katiba.
Hata hivyo wabunge wamekuwa wakiitetea hazina hiyo wakisema kuwa kuondolewa kwa hazina hiyo mikononi mwao kutakuwa pigo kwa wananchi wengi ambao wamenufaika kutokana na maendeleo yake.