HabariNews

Spika Kingi: “kaunti zisitegemee serikali kuu, zivumbue mbinu za uongezaji mapato”

Spika wa Bunge la Seneti Amason Jeffa Kingi amepongeza hatua ya serikali kutoa mgao wa takribani shilingi 3.3 trilioni kufanikisha maendeleo ya kaunti kwa manufaa ya mwananchi.

Akiongoea Jumatano Agosti 16 huko Eldoret kaunti ya Uasin Gishu kwenye Kongamano la Ugatuzi linaloendelea, Kingi alisema kwa kipindi cha miaka 10 bunge la seneti limekuwa mstari wa mbele kisheria na kuwajibikia masuala mbalimbali ya kisheria.

“Kwa miaka 10 iliyopita mchango wa bunge la seneti katika kufanikisha ugatuzi hauna mfano wake. Kupitia majukumu yake kisheria Seneti imetoa mwongozo na inasalia kuwajibikia majukumu yake,” alisema Kingi.

Wakati uo huo Kingi amehimiza serikali za kaunti kukumbatia mifumo mipya ya kuimarisha ugatuzi ikiwemo kushirikiana na wadau mbalimbali sawia na kuvumbua mbinu mpya za ukusanyaji mapato na kuacha kutegemea serikali kuu kwa asilimia kubwa.

“Tunataka kuona kaunti zikijukumika zaidi kutafuta ushirikiano muhimu zaidi na washikadau mbalimbali kufanikisha ugatuzi. Nazipa changamoto Kaunti lazima zivumbue mbinu za kuendeleza ugatuzi, mbnu zaidi za ukusanyaji mapato ili kuepuka kutegemea sana mgao wa Serikali Kuu,” alisema Kingi

Spika huyo aidha amekariri kuwa kaunti sharti ziwajibike vilivyo katika kufanikisha malengo na majukumu yao.

Naye Mwenyekiti wa magavana Anne Waiguru alipongeza rais William Ruto kwa kutoa mgao wa fedha za kaunti kwa wakati.

Waiguru alisema hatua hiyo imewezesha kaunti kufanya maendeleo yake kwa wakati.

Aidha waiguru alidokeza kuwa taifa bado linajikwamua kutoka kwenye hasara iliyokandiriwa wakati wa ugonjw wa korona na kuwahimiza Wakenya kuwa wavumilivu katika uongozi wa Raisa Ruto.

BY EDITORIAL DESK