HabariNews

Mahakama yasitisha Agizo la kufutilia mbali Kanisa la Pasta Ezekiel

Ni afueni kwa Mchungaji wa Kanisa na New Life Prayer Centre, Ezekiel Odero baada ya mahakama kuu kusitisha agizo la Msajili wa Vyama lililofutilia mbali usajili wa Kanisa lake.

Odero aliwasilisha ombi jipya siku ya Jumatatu, Agosti 21 na kuamua kuondoa lile la awali ambalo alikuwa amewasilisha mnamo Agosti 20.

Jaji Jairus Ngaah alitoa agizo hilo kwa nia ya kuhoji iwapo mchakato uliopelekea kufutiliwa mbali kwa usajili uliambatana na sheria na iwapo ulikuwa wa kisheria na haki kwa Odero.

Katika karatasi zake mahakamani, Odero amedai kuwa hakupewa nafasi yeyote ya kujitetea yeye na kanisa kabla ya Msajili wa Vyama kuanza kufuta usajili wa New Life Prayer Center na Kanisa.

Wakili wa Kasisi Odero, Danstan Omari aliomba uamuzi huo ubatilishwe kwani unawanyima waumini wake uhuru wa kuabudu.

“Inazidi kukatisha tamaa kutokana na majaribio mengi ya vyombo vya dola kunitesa, kukatisha huduma yangu na hatimaye sio tu kufunga Kituo cha Maombi ya New Life Prayer Centre bali pia miradi yangu mingine yote,” Alisema Odero.

Katika maombi hayo mapya ya Mchungaji Odero Jaji Ngaah alisema, “baada ya kuchunguzwa kwa nyenzo zilizowasilishwa mahakamani kuunga mkono ombi hilo, nimeshawishika kutumia busara na kuwaruhusu waombaji kupinga notisi ya gazeti la Agosti 18, 2023, ambayo madhumuni yake ni kufuta usajili. jamii inayojulikana kama New Life Prayer Center and Church.”

BY EDITORIAL DESK