Kuna matumaini makubwa viwango vya utalii Pwani na kote nchini kwa jumla vikaimarika maradufu kufuatia ujio wa meli ya kifahari yenye maktaba kubwa ya MV Logos Hope.
Kulingana na waziri wa utalii Peninah Malonza amesema kuwasili kwa meli hiyo yenye wahudumu zaidi ya 3000 na maktaba ya kisasa itainua pakubwa kiwango cha utalii kwa siku 45 ambazo meli hiyo itakakuwa hapa mjini Mombasa.
Kwenye hotuba yake alipoitembelea meli hiyo ya kifahari mnamo Jumatano, Agosti 23 katika eneo la Likoni Malonza aidha alisema kwamba mafunzo yatakayopeanwa kwa siku zijazo yataboresha utendakazi wa baharini.
“Meli hii ya maktaba inayoelea inatoa fursa kwa jamii yetu zaidi ya nafasi 500 za kujiendeleza kiutafiti wa kisayanasi, masuala ya ubaharia na sanaa, yote hayo kwa ada nafuu. Kando na masuala ya vitabu meli hii itaimarisha fursa za kuendeleza ubaharia, uchumi wa sekta ya utalii na hata kuuza vivutio vyetu vya utalii Kenya,” alisema Waziri Malonza.
Wakati huo huo Gavana wa Mombasa Abdulswamad Sheriff Nassir amesema kwamba kuwasili kwa meli hio ya kifahari kutawapa fursa wanafunzi wengi na wakazi wa Pwani kupata mafunzo ya kihistoria.
“Nikiwa mmoja wa wanaopenda kusoma licha ya kukosa muda kwa sasa japo nitatenga muda kuja kujisomea kiasi, kwa sababu hiyo ni jukumu langu kuhamasisha wengine kuja hapa. Meli hii ikiwa yenye vitabu ni fursa kwa wanafunzi na wakazi kusoma kujua mengi,” alisema Gavana Nassir.
Hii ni meli ya pili ya kifahari kutia nanga katika bandari ya Mombasa baada ya Doulos kuzuru Kenya mwaka wa 2005.
Inaarifiwa kuwa Meli hiyo itafungua milango yake kwa umma kwenda kujisomea kuanzia Alhamisi Agosti 24, kwa kiingilio cha shilingi 50.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali ikiwemo seneta wa kaunti ya Mombasa Mohammed Faki miongoni mwa wengineo.
BY MJOMBA RASHID.