Habari

Ongezeko la kihistoria! EPRA na Bei mpya za mafuta wazua tumbojoto Nchini

Wakenya wameendelea kutoa hisisa zao kuhusiana na ongezeko la bei ya mafuta iliyotangazwa usiku wa kuamkia leo Ijumaa.

Mamlaka ya Kudhibiti Kawi na Mafuta ya Petroli EPRA imeongeza bei za mafuta kwa takribani shilingi 20 kwa lita ongezeko ambalo limevuka rekodi ya shilingi 200 kwa mara ya kwanza katika historia ya Kenya.

Wakenya wakionyesha ghadhabu yao katika mitandao ya kijamii kufuatia mabadiliko hayo wameeleza kutamaushwa na jinsi gharama ya maisha inavyozidi kuwaumiza.

Wengi wametaja ongezeko hilo kuwa litakalozidi kumwumiza mwananchi wa kawaida, baadhi ya wakenya wakimrai kiongozi wa upinzani Raila Odinga kuingilia kati ili kuwanasua kutokana na hali hii ilivyo.

Akijibu chapisho la Mwanamkakati wa Kidijitali Dennis Itumbi katika mtandao wa X Mkenya mmoja aliandika, “Huwezi kulinganisha Kenya na mataifa ya nje kwa masuala ya bei za mafuta, kama ni hivyo tuangaliie pia gharama ya maisha ya huko.”

@Omwamba aliandika, “Sisi hatuna nchi! Tunaelekea wapi kama taifa?” Aliuliza

“Wueh! Ni kubaya, wangerudisha tu ruzuku, kwani subsidy si ilimaanisha that extra cost was met by our tax, ama ilikuwa aje?” Aliandika mmoja

Kulingana na EPRA bei ongezeko hilo ni kufuatia kupanda kwa bei hizo katika soko la Kimataifa, na hapa nchini Mafuta aina ya petrol yamepanda kwa takribani shilingi 17 kwa lita, dizeli ikipanda kwa shillingi 21.32 na lita ya mafuta taa kwa shillingi 33.13.

Hapa Mjini Mombasa mafuta ya petrol yatauzwa kwa shilingi 208.58 kwa lita, Dizeli shilingi 197.93 nayo mafuta ya taa yakiuzwa kwa shilingi 199.54 na huko jijini Nairobi Petrol itauzwa kwa shilingi 211.64, Dizeli kwa 200.99 na mafuta ya taa kwa shilingi 202.61.

Bei hizi mpya zimetangazwa baada ya serikali kutangaza kuondoa ruzuku ya baadhi ya bei ya bidhaa muhimu hapa nchini.

NA MJOMBA RASHID