Mtu mmoja ameripotiwa kuuawa na zaidi ya nyumba 7 kuteketezwa moto eneo la Widhu wadi ya Mkunumbi huko kaunti ya Lamu mapema Septemba 20, 2023.
Inaarifiwa kuwa watu walioaminika kuwa wanachama wa kundi la Al-Shabab walitekeleza uvamizi huo ambapo kabla ya kutia moto nyumba hizo walimwua mlinzi wa shule ya msingi ya Majembeni.
Vijiji vya Widhu, Salama na Juhudi vilivyoko maeneo ya vijijini vya kaunti hiyo vimekuwa vikikumbwa na mashambulizi ya kigaidi kutoka kwa kundi la kigaidi la alshabab jambo lililowalazimu wengi kuhama makazi yao kwenda maeneo salama.
Ndani ya kipindi cha miezi minne, vijiji hivi vilikumbwa na mashambulizi zaidi ya sita yaliopelekea watu zaidi ya 10 kupoteza maisha na mali kuharibiwa.
Shambulio hili la leo lilijiri tu baada ya Waziri wa usalama wa ndani na masuala ya kitaifa Prof. Kithure kufanya kikao na maafisa wa usalama katika kaunti hiyo ya Lamu.
Itakumbukwa kuwa ni siku kadhaa baada ya Waziri Kindiki kudokeza kuwa maafisa wa usalama wa maeneo ya Kaskazini mashariki na yanayokumbwa na uvamizi wa wanamgambo wa alshabab kupewa silaha za kisasa ili kukabiliana na utovu usalama katika maeneo hayo.
BY EDITORIAL DESK