HabariNews

NACADA Kushirikiana na Viongozi wa Kidini kukabili mihadarati kaunti ya Kwale

Mamlaka ya kupambana na utumizi wa pombe na dawa za kulevya nchini (NACADA) sasa inalenga kushirikiana na viongozi wa kidini ili kukabiliana na tatizo la mihadarati katika kaunti ya Kwale.

Afisa wa Mamlaka hiyo tawi la Kwale Lucy Wanjiku alisema kuwa wanapania kushirikiana na viongozi wa makanisa na misikiti ili kukomesha utumizi wa dawa za kulevya katika eneo hilo

“Dawa ya kulevya inayotumika zaidi Pwani na nchini ni pombe na bangi, Ni muhimu tuhimize watoto wetu kujihusisha na mambo ya kiimani, kama Sunday school, kama ni madrasa wafundishwe ile pia inakuwa ni kinga kwao. Ndio maana sisi kama serikali tunashirikiana na vitengo tofauti ikiwemo viongozi wa kidini kukabili vita hivi,” alisema Bi. Wanjiku.

Haya yamejiri kufuatia uzinduzi wa kitabu maalum cha kukabiliana na mihadarati katika jamii kupitia mradi wa Faith Community Against Drug Abuse (FACADA) unaotekelezwa na kanisa la FPFK huko Diani.

Afisa msimamizi wa mradi huo Emmanuel Kahaso alisema kuwa kitabu hicho kitapiga jeki juhudi za viongozi wa kidini kulikabili tatizo hilo kikamilifu.

“Tulifanya utafiti tukakuta viongozi wa kidini hawana taarifa za kutosha hawaelewi, na zile sehemu wakatuelezea tukaona tutafute taarifa ambazo hawana tuziweke kwenye kitabu kiwe kama reference kupata taarifa wanapokuwa nyanjani kiwasaidie maana walikuwa hawajui aina ya dawa na madhara yake,” alisema Bw. Kahaso.

Kulingana na utafiti wa NACADA uliofanywa mwaka 2022, utumizi wa mihadarati umekithiri mno katika eneo la Pwani huku watoto wenye umri wa kuanzia miaka 6 wakitumia pombe na sigara.

BY MJOMBA RASHID