Vuguvugu la viongozi wa Jamii za Asili kaunti ya Lamu wamekashifu kauli ya Seneta wa kaunti ya Nyeri Wahome Wamatinga akidai kuwa jamii hizo zimekuwa zikitekeleza mashambulizi ya kigaidi yanayoshuhudiwa kaunti hiyo.
Wakihutubia wanahabari hapa mjini Mombasa siku ya Ijumaa Septemba 22, viongozi hao walieleza kughadhabishwa na matamshi hayo wakitayataja kuwa ya uchochezi na yenye kulenga kusambaratisha amani baina ya jamii zinazoishi kaunti hiyo.
Viongozi hao Walisema kuwa hatua hiyo inalenga kuyumbisha utawala wa gavana wa kanuti hiyo huku wakidai kuwepo kwa njama fiche ya kunyanyasa jamii zenye idadi ndogo ya watu nchini.
“Huyu bwana kusema kweli ametukosea sana na hakumkosea tu Gavana wetu ameikosea kaunti ya Lamu yote.”Akasema mmoja wa viongozi hao, Sultan Omar Shariff.
“Hii mipango yataka kutuumiza sisi makabila madogo na tunawaambia hilo halitapatikana Abadan.”Aliongeza mwenzake.
Kwa upande wake Mshauri wa vuguvugu hilo Hassan Albeit ambaye pia ni naibu mwenyekiti wa chama cha PAA amesema kauli hiyo inapania kutatiza miradi ya maendeleo iliyoelekezwa katika kaunti hiyo huku akiitaka serikali kuingilia kati ili kufanikisha mipango hiyo.
“Rais Ruto tumeuona utendakazi wako,Kindiki amekuja zaidi ya mara nne na amekaa na watu wote,na ameanza kutoa suluhisho.Hili suluhisho kutaka kupatika kumeruka watu wengine wataka kulivunja.Serikali ichukue hatua ya haraka sana kwa sababu mradi wa Lapset ni kubwa na watu wanataka kuwekeza.”Alisema Albeit.
Vilevile wameitaka serikali kupitia wizara ya usalama wa ndani kuwachukulia hatua za kisheria viongozi wanaochochea uhasama baina ya jamii nchini huku wakimtaka seneta wamatinga kuwasilisha ushahidi wa kuthibitisha madai yake.
Pia wameitaka serikali kutafuta mbinu za kukabili wanamgambo wa kundi la Al shabab wanodaiwa kutekeleza mashambulizi hayo wakihimiza wakaazi wa kaunti iyo kushirikiana katika mchakato wa kupata suluhu ya swala hilo.
“Tunatoa wito kwa serikali hususan waziri wa usalama wa ndani profesa Kithure Kindiki kuwachukulia hatua viongozi wanaochochea migogoro ya kikabila katika kaunti ya Lamu.Pia tunahimiza serikali kukabiliana na wanamgambo wa kundi la Al shabaab ili kuinua uchumi wa kaunti hiyo.”Alikariri Wakili Yusuf Abubakar.
Haya yanajiri baada ya seneta wa kaunti ya Nyeri Wahome Wamatinga akiwa katika bunge la seneti kudai kuwa jamii za asili kaunti hiyo zimekuwa zikitekeleza mauaji hayo yanayolenga kuwamaliza jamii zengine wakipata msukumo na uungwaji mkono kutoka kwa Gavana wa kaunti hiyo.