Shughuli za kusaka mwili wa mvuvi zinaendelea mjini Kilifi baada ya mashua yao kuzama Jumamosi 23, 2023.
Kulingana na msimamizi wa wamiliki wa mashua katika bandari ya Old Ferry mjini Kilifi Shallo Issa, wavuvi hao waliokuwa wanne kwenye mashua MV TUPENDANE, walizama maji eneo la Baobab baada ya mashua yao kupigwa na mawimbi makali na kuzama walipokuwa wakiendeleza shughuli zao za uvuvi.
Kulingana na Issa wavuvi wawili walinusurika kifo baada ya kufanikiwa kuogolea hadi ufuoni na wengine wawili wakizama kutokana na mawimbi makali . Issa alieleza kuwa walifanikiwa kuupata mwili wa mvuvi mmoja uliopatikana ukielea ufuoni mwa bahari hindi.
Wavuvi hao kwa ushirikiano wa usimamizi wa bandari ya Old Ferry mjini Kilifi na kitengo cha kukabiliana na dharura baharini wanaendeleza shughuli za kutafuta mwili wa mvuvi wa pili.
Hata hivyo issa alitoa wito kwa wavuvi kusitisha shughuli za uvuvi iwapo mawimbi makali yatashuhudiwa baharini ili kuepuka maafa zaidi.