Wadau mali mbali wametoa kauli za kuunga mkono mapendekezo ya mwenyekiti wa kamati ya bunge la kitaifa kuhusu Elimu Julius Melly kuwa wanafunzi waliolazwa hospitalini wakati wa mitihani ya kitaifa wasipelekewe mitihani hiyo mpaka pale watakapopona.
Naibu katibu mkuu wa walimu wa shule za upili na vyuo vya kati nchini KUPPET kaunti ya Kilifi Opollo K’Opollo,aliunga mkono pendekezo hilo akisemakuwa wanafunzi wengi wamekuwa wakifanya mitihani ya kitaifa wakiwa wamelazwa hospitalini na kuwapelekea kufeli mitihani hiyo.
K’Opollo Aliongeza kuwa hali hiyo iwakosesha wanafunzi wengi nafasi za kujiendeleza kimasomo kufuatia kufanya mitihani hiyo katika mazingira yasiyo sawa jambo analodai kuwa linawanyima usawa wanafunzi, wakati wa kufanya mitihani hiyo.
Alielezea hofu yake ya kutatizika kwa ratiba ya mitihani ya kitaifa kutokana na kutarajiwa kwa mvua ya El-Nino maeneo mengi ya nchi huku akitoa wito kwa baraza la mitihani nchini KNEC kuweka mikakati ya kuhakikisha mitihani ya kitaifa inawafikia wanafunzi kwa wakati.
Mitihani ya kitaifa inatarajiwa kuanza mwezi Oktoba na kutamatika mwezi Novemba.