HabariNewsSiasa

Msajili wa Vyama vya Kisiasa ahimiza usawa wa kijinsia katika vyama vya Kisiasa

Mkurugenzi mkuu wa usajili wa vyama vya kisiasa Anne Nderitu amewahakikishia Wakenya kuwa wameweka mikakati ikiwemo utumizi wa mtandao wa kidijitali wa E-citizen katika shughuli za kujisajili na kujiondoa kwenye vyama vya kisiasa.

Akizungumza mnamo Ijumaa Septemba 29, katika ufunguzi wa Ofisi ya usajili wa vyama vya kisiasa mjini Mombasa Nderitu alisema hatua hiyo itafanikisha ajenda za kila mmoja anayetaka kujiunga ama kujionodoa kwenye chama.

Nderitu alihimiza kila Mkenya kujiunga na chama chake anachokipenda kama njia ya kujihusisha na maendeleo lakini kwa kufuata sheria walizokubaliana wakati wa kujisajili kwenye chama hicho ikiwemo kuandika ilani au notisi kabla ya kujitoa.

”Lazima ufuate mikakati ambayo ulikubaliana nayo na kuweka sahihi kwamba wewe ni mwanachama pia hivyo wakati wa kutoka lazima ufuate mikakati hiyo, kupeana notisi ya kuonyesha kuwa umetoka.” Alisema Nderitu.

Nderitu amehimiza vyama kuwa na wagombea wengi kwa kuzingatia usawa wa kijinsia ili kupata mgao wa fedha kwenye vyama hivyo kama njia ya kukuza vyama hivyo.

“Ili chama kipewe pesa lazima kiwe na mtu mmoja ambaye amechaguliwa katika hicho chama, na kuangalia chama kilipata kura ngapi halafu kizingatie usawa wa jinsia wanawake vijana na walemavu.” Alikariri.

Kwa upande wake msaidizi wa usajili wa vyama vya kisiasa Florence Birya alihimiza kila Mkenya kujisajili katika chama cha kisiasa ili kutimiza haki yake ya kikatiba akiongeza kuwa taifa limeruhusu vyama vingi.

“Katika katiba ya Kenya kifungu cha 38 kila mkenya ana haki ya kuwa kwenye vyama vya kisiasa na hatuwezi kufurahia haki hiyo iwapo hatutakuwa kwenye vyama vya kisiasa kwa hivyo ni muhimu kuwa katika vyama vya kisiasa.” Alisema Birya

BY MEDZA MDOE