HabariLifestyleMombasaSiasa

Serikali kuu yashinikizwa kuwapa uhuru Magavana kutekeleza wajibu wao

Serikali kuu imeshinikizwa kuwapa uhuru magavana kutekeleza wajibu wao bila kuwaekea vikwazo vyovyote ili kuboresha utendakazi wao.

Akihutuhubia wanahabari mjini Mombasa Kinara wa Azimio Raila Odinga alieleza baadhi ya changamoto zinazokumba magavana katika harakati ya kuendesha shughuli zao, ikiwemo kuingiliwa na kucheleweshwa kwa fedha za kaunti kutoka serikali kuu, huku akiwataka kupewa uhuru wa kufanya maamuzi yanayoambatana na kaunti zao.

Aidha Odinga aliitaka serikali kuu kushirikiana na serikali za kaunti kufanikisha ajenda za maendeleo kwa manufaa ya wananchi.

“Jaribio la serikali kuu kuchukua baadhi ya majukumu ya serikali za kaunti ni mojawapo ya changamoto kuu.Huku magavana wakijitahidi kutekeleza wajibu wao kulingana na katiba,serikali ya kitaifa inajaribu kudidimiza utendakazi wao.Serikali kuu inapaswa kuheshimu katiba na kuacha kuingilia kazi ya serikali za kaunti.”alisema Odinga.

Vilevile aliongeza kuwa licha ya mazungumzo ya maridhiano baina ya serikali na upinzani kuendelezwa, katu hawatasitisha juhudi za kuwatafutia haki waathiriwa wa ukatili wa maafisa wa usalama wakati wa maandamano ya upinzani.

Wakati huo huo alitilia shaka mchakato wa kubinafsishwa kwa sehemu ya bandari ya Mombasa akiutaja kuwa wa siri akisema kuwa  mpango huo haukuhusisha wakaazi na viongozi wa kaunti hiyo akisisitiza kuwa wanapinga hatua hiyo.

“Lengo la kubinafsisha Bandari ya Mombasa na serikali kuu bado halijawekwa wazi na hatujaridhishwa na uamuzi huo ambao haukuhusisha wakaazi na viongozi wa kaunti ya Mombasa .Mrengo wa Azimio unapinga kutekelezwa kwa suala hilo.”alikariri Odinga.

 

BY NEWS DESK