HabariNews

Maadhimisho ya Sikukuu ya Utamaduni, Wakenya watakiwa kutumia Utamaduni kueneza amani

Taifa la Kenya limeadhimisha Siku ya Utamaduni, zamani ikujulikana kama Moi Day huku Wakenya wakihimizwa kuukumbatia na kutumia utamaduni wao kama njia mojawapo ya kuleta amani.

Sikukuu hiyo ambayo ilibadilishwa jina mara kadhaa tangu miaka ya 80 iliadhimishwa kitaifa kwa mara ya kwanza baada ya zaidi ya mwongo mmoja kuhangaika kutafuta jina na maana mwafaka ya sikukuu hiyo.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Utamaduni katika ukumbi wa Bomas jijini Nairobi, mnamo Jumanne Oktoba 10, Waziri wa Utumishi na Huduma za umma Moses Kuria alieleza haja ya utamaduni kutumiwa kuleta amani hapa nchini hususan katika maeneo yanayokumbwa na vurugu na utovu wa usalama.

Kuria alisema utambulishaji wa tamaduni kwa wakenya kutawezesha kufahamu jinsi watu wa kale walivyotangamana na kusuluhisha migogoro tofauti tofauti.

“Tutumie utamaduni kwa kuleta amani na ustawi, zamani mababu zetu walifahamu muda gani wa amani na wakati wa kuingia vitani. Ninapotazama maeneo kama Kapedo, Bonde la Kerio na Lamu ambako kumekuwa na ukosefu wa salama, kama tungetumia taasisi zetu za tamaduni kutatua matatizo haya tungeleta amani nchini na kusaidia pakubwa kupunguza gharama za kukabiliana na ukosefu wa amani na usalama,” alisema Waziri Kuria.

Naye Katibu mkuu wa Wizara ya Utamaduni na Turathi, Ummi Bashir ameweka wazi mpango wa kuweko kwa vazi rasmi la kitaifa ili kuonyesha mila, kuleta ladha ya makabila na utamaduni.

 

“Kenya hatuna vazi la kitaifa. Ni suala ambalo tunalifanyia kazi na tunaahidi Sikukuu ijayo ya Utamaduni tutakuwa na vazi la kitaifa kudhihirisha Utamaduni wetu, tutashirikisha na kushauri wadau wote ili umoja na amani wetu udumu, Kenya yetu amani, umoja na upendo,” alisema Bi. Bashir huku akipokea pongezi kwa waliohudhuria.

 

Kwa upande wake mke wa rais Bi. Rachael Ruto ambaye pia amehudhuria hafla hiyo amesema kwamba Siku ya Utamaduni ni siku ambayo inawaunganisha wakenya ili kufurahia utamaduni.

“Ni siku kwetu sisi kuungana na kufurahia utofauti wa makabila yaliyopo kuwa kitu kimoja. Kauli mbiu kuwa ‘Utamaduni, twajivunia utangamano’ unajumuisha kiini cha mkusanyiko wetu leo, inaashirikia utamaduni wetu, tunajivunia uelewano wetu. Utamaduni wetu unatutambulisha sisi ni nani na unatuunganisha katika jumuiya ya kimataifa.” Alisema Bi. Rachel.

MKuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei alitoa changamoto kwa wakenya kuwa mstari wa mbele kujifahamisha tamaduni mbali mbali, akibaini kuwa serikali inachukulia kwa umuhimu mkubwa masuala ya tamaduni kwa kuwa utamaduni ni mojawapo ya vitambulisho vikuu vinavyotambulisha taifa hili.

Maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Utamaduni awali ikijulikana kama Moi Day, yamefanyika katika ukumbi wa Bomas na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali.

Kabla ya kuafikiwa kuwa Siku ya Utamaduni, mnamo mwaka 2019 rais mstaafu Uhuru Kenyatta kupitia baraza lake la mawaziri aliidhinisha kubadilishwa kwa jina kutoka kwa Siku ya Moi hadi Siku ya Huduma, ikimaanisha utoaji huduma zaidi kama ilivyokuwa uhalisia wa siku yenyewe wakati wa uongozi wa rais hayati Daniel Moi.

Mwaka mmoja baadaye siku hiyo ilifanyiwa mabadiliko na kuwa siku ya Utamaduni.

MJOMBA RASHID