Bunge la kitaifa limeongezea muda wa siku 30 kamati ya Jopo la mazungumzo ya kitaifa ili kukamilisha majukumu yake ipasavyo.
Spika wa bunge la kitaifa Moses Wetangula ametoa uamuzi huo katika vikao vya bunge vya Jumanne Oktoba 17.
Hii ni baada ya jopo hilo kuomba siku 30 zaidi ili kukamilisha vikao vyake ambapo jopo hilo linajumuisha watu kumi kutoka mrengo wa upinzanin wa Azimio na ule wa Kenya Kwanza.
Aidha Kinara wa wengi katika bunge la kitaifa Kimani Ichungwah aliwasilisha ombi hilo mapema Jumanne ili kuomba bunge iwaongeze muda zaidi ili kukamilisha vikao vyake na kuwasilisha ripoti kamili bungeni tarehe 26 Novemba mwaka huu.
Kufikia sasa jopo hilo limeafikiana kufanyiwa ukaguzi matokeo ya uchaguzi wa urais wa mwaka 2022, kubuniwa kwa ofisi ya kiongozi wa upinzani na waziri mwenye Mamlaka makuu, kuangaziwa upya kwa mchakato wa kuwateua wanachama wa jopo la makamishina wa IEBC na kuwepo kwa uhuru wa vyama vya kisiasa nchini.