Huku ulimwengu ukiadhimisha siku ya uhamasisho kuhusu jamii ya huntha ‘Intersex persons’, wanajamii eneo la Pwani na Taifa zima kwa ujumla wamehimza kuwakubali watu wa jinsia mbili na kulinda haki zao.
Mwanachama wa Jopo kazi la kutekeleza sheria ya watu waliozaliwa na jinsia mbili (huntha) Faiza Musa ambaye pia ni wakili katika tume ya kitaifa kutetea haki za binadamu KNCHR, alisema kuwa watu wa jinsia mbili walitambuliwa kisheria mwaka wa 2022 na ni sharti jamii iwakubali akiongeza kuwa ni maumbile ya mwenyezi Mungu wala sio mapenzi yao.
Faiza aliwahimiza wazazi kutochukua hatua ya kuwafanyia upasauaji watoto wakiwa wadogo kabla ya watoto hao kujulikana jinsia zao baada ya kubaleghe, akidokeza kuwa hatua hiyo huwatatiza mbeleni hasa wakati wanapohitajika kuanzisha familia.
“Wazazi wasiweze kufanya zoezi la upasuaji mapema kwa sababu maisha ambayo anaishi na mtoto ni mfupi mwaka 1mpaka 18 baada ya hapo anamaisha yake na huenda akakosa kuwa na familia kwa sababu ya mabadiliko ya homoni kadri anavyokua.”Alisema Faiza.
Kulingana na Faiza ipo haja kuu ya mswada wa watu wa jinsia mbili kupitishwa bungeni ili kuwapatia fursa ya kuishi kama watu wengine humu nchini na kuepuka unyanyapa na ubaguzi kwa watu wa jamii hii.
Mswada huo uliozinduliwa mwaka huu unajumuisha usajili wa alama ya I katika stakabadhi mbali ikiwemo cheti cha kuzaliwa pamoja na vyeti vya shule huku akisisitiza kuwepo na urahisi wa vyeti hivyo kufanyiwa mabadiliko kadri mtoto anavyokuwa.
“Tulikuja na huo mswada wa watun wa jinsia mbili Huntha na mswada huo unaangazia iwe rahisi kwa mwana Huntha kuishi kama mtu wa kawaida ikiwemo usajili wakati wa kuzaliwa kuwepo na alama ya I sawia na ile ya mume (M) na Mke(F) na hata urahisi wa kubadilisha vyeti hivyo kadri anavyokuwa iwapo kuna mabadiliko ya homoni.” Alisema Faiza.
Itakumbukwa kuwa zoezi la sensa za mwaka 2019 lilibaini kuwa Kenya ina huntha 1,524 idadi ambayo ni asalimia 0.3 ya idadi ya jumla ya wakenya nchini humo.