Huku watahiniwa wa darasa la 8 wakitarajiwa kufanya Mitihani yao ya Kitaifa KCPE kuanzia juma lijalo, Serikali ya kaunti ya Mombasa imebaini kuwa itawasimamia chakula cha mchana wakati wa mitihani hiyo.
Akizungumza katika ukumbi wa shule ya upili ya wasichana ya Jomvu Gavana wa Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir amepigia upatu mpango huo akieleza matumaini ya wanafunzi kufanya vyema katika mitihani.
Nassir alisema kuwa mpango huo wa lishe kwa watahiniwa wakati wa mitihani unanuia kuwapa watahiniwa utulivu na kumrahisishia mzazi akisema kuwa wengi hutatizika na njaa wakati wa mtihani hususani wale wanaotoka katika familia zisizojiweza.
Aidha Nassir amewataka wazazi kuhakikisha kuwa wanawatayarisha vyema watoto wao akieleza kuwa hakuna mzazi atakaye gharamika kumlipia mtoto wake chakula cha mchana wakati wa mtihani.
“Serikali ya Kaunti ya Mombasa itasimamia mpango wa chakula kwa watahiniwa wa darasa la 8. Tuhakikishe hakuna mzazi atatozwa malipo yoyote kwa ajili ya mpango wa chakula kwa watahiniwa hao na ikiwa mzazi alilipa hiyo pesa basi apewe mtoto wake atumie baada ya mtihani huo, Tutasimamia watahiniwa wote wa darasa la nane kutoka Kaunti ya Mombasa,” Alisema Gavana Nassir.
Watahiniwa wa darasa la 8 wanafanya maandalizi ya mwisho ya mtihani maarufu ‘rehearsals’ Ijumaa hii kabla ya kuanza rasmi mitihani yao siku ya Jumatatu juma lijalo.
Kutoka Meza ya Habari ya Sauti ya Pwani tunawatakia watahiniwa wote wa mwaka huu 2024 KILA KHERI!
BY MJOMBA RASHID