HabariNews

Shinikizo kwa kaunti ya Lamu, Wawakilishi wadi wakiibua maswali kuhusu miradi kadhaa

Kitendawili kuhusu utekelezwaji miradi mbalimbali ya kaunti ya Lamu kimegubika kaunti hiyo huku Wawakilishi wadi wa kaunti hiyo wakiibua maswali mazito bungeni.

Mwakilishi mteule katika bunge la Lamu Zahara Shee alimtaka Mwenyekiti wa Idara na kamati ya utoaji wa huduma za afya, maji na mazingira kuelezea mipango iliyowekwa na idara hiyo kuondoa majitaka yaliyozagaa katika mji wa Lamu.

Mwakilishi huyo aliibua maswali bungeni akitaka kujua mikakati iliyo nayo kaunti hiyo ya kuzibua mabomba yote ya majitaka sawia na mipango ya kudumu kuzuia kuziba kwa mabomb hayo.

Kuhusu masuala ya elimu Mohammed Aboud ambaye ni Mwakilishi wadi ya Faza aliibua maswali kwa mwenyekiti wa Kamati ya idara ya elimu, tamaduni, na ustawi wa jamii akitaka kujua ukumbi wa Faza na Pate utafunguliwa lini rasmi.

Kwa upande Mwakilishi wadi ya Bahari Francis Gakonga ameibua maswali kwa kamati ya Idara ya uchukuzi na kazi za umma akitaka kujua kwa nin barabara za Mkunumbi na Mpeketoni zimechukua muda mrefu kukamilika na shughuli ya kuzikamilisha itafikia mwisho lini.

Kuhusu visa vya wizi na ubakaji vilivyoripotiwa kaunti hiyo, Mwakilishi Mteule Aisha Abdulrahman aliibua maswali kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Idara ya Utendakazi wa baina ya Serikali Kuu na ya Kaunti akitaka kujua mipango iliyowekwa kukabiliana na visa hivyo vinavyotishia usalama na haki za watoto na kijinsia.

Aidha Mwakilishi wadi huyo alitaka majibu kwa serikali ya kaunti iweke bayana kuhusu mikakati waliyoiweka kutoa hakikisho la usalama kwa watoto na jamii ya kaunti hiyo kwa jumla.

Kwa sasa Bunge la kaunti ya Lamu limevunja vikao vyake na linatarajiwa kurejelea vikao hivyo Jumanne ya tarehe 31 mwezi huu wa Oktoba siku ambayo majibu ya masuala yote yaliyoibuliwa yatawasilishwa kwenye bunge hilo.

BY MJOMBA RASHID