HabariMombasaNews

Mombasa Kuanza kupokea Safari za Ndege za Kimataifa Januari 2024

Usafiri wa Ndege za moja kwa moja kutoka mataifa ya nje kuja mjini Mombasa sasa unatarajiwa kuanza Januari mwakani. Haya ni kwa mujibu wa Gavana wa Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir.

Akizungumza eneo bunge la Nyali kwenye kongamano lililowaleta pamoja wadau katika sekta ya biashara nchini Gavana Nassir alisema kuwa ndege za kwanza zitakazoingia hapa Mombasa ni za kutoka Dubai ambazo zitaanza kuanzia tarehe 14 Januari.

Nassir alibaini kuwepo kwa mfumo wa Anga huru ‘Open Sky Policy’ kutawawezesha watalii wengi kuzuru eneo la Pwani hivyo basi kuimarisha uchumi wa Pwani na hata kuimarika kwa biashara.

“Nina furaha kusema kuwa kuanzia Januari mwakani ndege za Fly Dubai itakuwa ikifanya safari 4 za ndege kila wiki kuja hapa Mombasa, kuanzia tarehe 14 au 17 Januari 2024. Lufthansa tayari inafanya hayo na Ethiopian Airlines na tuna imani mashirika mengi zaidi,” alisema Nassir.

Hata hivyo Nassir amesema serikali ya kaunti ya Mombasa pamoja na washikadau mbalimbali itazidi kuishurutisha serikali Kuu kuruhusu ndege zote kutoka mataifa mengine kutua moja kwa moja Mombasa.

“Tuna majadiliano kuhakikisha kuwa mashirika mengine ya ndege kimataifa yanafanya safari zake moja kwa moja kuja hapa. Kama vile Qatar, Turkish na Rwanda haya yote na mengine ndege zao zije hapa kuendeleza biashara. Tumekuwa tukihimiza Mfumo kamilifu wa Anga huru,” alisema.

Nassir aidha alisema Mombasa sasa iko huru kuendesha shughuli aina ainati za biashara.

BY MJOMBA RASHID