Uncategorized

Kesi Inayomuandama Mchungaji Ezekiel Odero bado Haijafungwa, Asema Igonga.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Renson Ingonga ameweka wazi kuwa kesi inayomuandama Mchungaji Ezekiel Odero bado haijafungwa.

Kulingana na naye ni kuwa uchunguzi wa suala hilo bado unaendelea na kuwa Hakimu Mkuu Mwandamizi Joe Omido alifunga faili ya hifadhi kwenye kesi hiyo. Aidha aliongeza kuwa ODPP itachukua hatua mwafaka pindi uchunguzi utakapokamilika.

Mnamo siku ya Jumanne Oktoba 31, Jaji Omido katika uamuzi wake alisema hakuwa na chaguo jingine ila kuisitisha kesi hiyo mara moja na kumwondolea mashtaka Ezekiel baada ya kutathmini kwa kina maombi ya mshtakiwa na utetezi wa kesi hiyo.

Kufuatia ushahidi na stakabadhi za pande zote zilizowasilishwa mbele ya mahakama hii, sina namna nyingine ila kuiondoa kesi hii, na naagiza arejeshewe milioni 1.5 alizotoa kama dhamana,” alisema Jaji Omido.

Haya yanajiri kufuatia Mahakama ya Shanzu kutupilia mbali kesi inayomuandama Mhubiri Odero baada ya miezi kadhaa tangu kesi hiyo kuwasilishwa mahakamani na kuamuru kurejeshewa kima cha shillingi millioni 1.5 alichokuwa ametoa kama dhamana.

Pasta Ezekiel kama anavyojulikana na wengi, alishtakiwa kwa tuhuma za mauaji, utekaji nyara, kueneza itikadi kali kwa waumini wa kanisa lake na utakatishaji wa fedha miongoni mwa makosa mengine.

Mawakili wa Odero wakiongozwa na Cliff Ombeta naye Danstan Omari walikuwa wameitaka Mahakama kuharakisha mchakato wa kesi hiyo kwa kile walichodai mchakato wa kesi hiyo kuchukua muda mrefu pasi kuamuliwa wala kuendelezwa kwa kesi.

Akizungumza muda mfupi baada ya hukumu kutolewa na mahakama ya Shanzu iliyomwondolea mashtaka, Pasta Ezekiel kama anavyojulikana na wengi alieleza furaha yake ya kuondolewa kesi hiyo akisema kuwa mashtaka dhidi yake yalilenga tu kumdhalilisha.

Hata hivyo Odero alisema kuwa hana chuki wala hasira yoyote na serikali wala idara yoyote kuhusiana na madai ya kesi yaliyokuwa yakimkabili.

BY MJOMBA RASHID