HabariNewsUncategorized

Serikali Kulipa Deni la Dola Bilion 2 za Eurobond kwa awamu kuanzia mwezi Disemba

 

Kenya sasa itaanza kulipa kwa awamu deni lake la Dola bilioni 2 za Eurobond inayodaiwa katika mwezi Disemba mwaka huu.

Kwenye hotuba yake ya kwanza ya taifa katika majengo ya bunge mnamo Alhamisi rais William Ruto alitangaza kuwa deni hilo la dola bilioni 2 za marekani sawia na bilioni 304 za Kenya zitalipwa kwa awamu ya kima cha dola Milioni 300 (shilingi bilioni 45.6).

Rais alikariri kuwa historia ya taifa kuendelea kukopa imefungia nje sekta ya umma ya taifa katika masoko ya fedha na hasa ikiongeza gharama ya mikopo na kukwamisha biashara na uchumi.

Juhudi zetu za kuimarisha hali hiyo imezaa matunda na mwezi ujao wa Disemba tutaweza kulipia kwa awamu malipo ya kwanza ya dola milioni 300 za deni la Eurobond ambalo muda wake wa kulipa unaisha mwaka ujao. Kwa kujiamini tutalipa deni hilo ambalo limekuwa chanzo cha kero kwa Wakenya, soko na Washirika wetu,” alisema rais.

Alisema kuwa baada ya kuchukua uongozi wa taifa serikali ya Kenya Kwanza ililazimika kufanya maamuzi magumu ya kiuchumi ili kulikwamua kwa kuweka imara uchumi wa taifa uliokuwa ukiporomoka kwa kasi, hatua ambazo amedai zinaanza kuzaa matunda.

Imetubidi kuchukua maamuzi magumu na kufanya maamuzi chungu nzima kwa sababu tuna deni kwa Wakenya kufanya jambo sahihi na kukabiliana na ukweli jinsi ulivyo bila kukurupuka au kusawazisha,” alisema.

Rais Ruto alisema serikali imeanzisha mageuzi ya kimapinduzi yanayolenga kudhibiti deni la nchi ili kuhakikisha kuwa taifa linaishi kulingana na uwezo wake, na kupitia mageuzi na maamuzi hayo magumu mashirika ya kimataifa sasa yana imani na taifa.

BY MJOMBA RASHID