HabariNews

KWAHERI KCPE! Kila lenye mwanzo lina mwisho, Pazia za KCPE zafungwa baada ya miaka 39

Kufuatia kutangazwa kwa matokeo ya mtihani wa kitaifa wa darasara la nane KCPE, sasa ni rasmi mapazia ya mfumo wa elimu wa 8-4-4 katika shule za msingi yanafungwa.

Mtihani wa KCPE uliofanywa kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 1985 baada ya kuchukua nafasi ya mtihani wa kitaifa CPE, utasalia kwenye kumbukumbu nzuri ya usambamba wa safari na safari ya usambamba ya mtaala ambao umeendesha elimu ya msingi nchini kwa miaka 39.

Mnamo 1981, jokopokazi maalum lilipewa jukumu la kuchunguza mtaala wa elimu nchini wakati huo na hatimaye kamati hiyo iliwasilisha pendekezo la kubadili mfumo wa elimu wa 7-4-2-3 hadi mfumo wa elimu wa 8-4-4, ambao muundo wake wa jumla ulikuwa sawa na mfumo wa elimu wa Marekani.

Na licha ya changamoto za utekelezwaji wa mfumo wa huo mpya, mfumo wa 8-4-4 ulikusudia kusisitiza sana maandalizi ya kimtazamo na ujuzi wa mahali pa kazi,sera ambayo ilinuia kuboresha uwezeo na ufanisi wa wanafunzi kimasomo.

Mtaala wa 8-4-4 ulilenga kutoa mafunzo kwa muda wa miaka Minane kitengo cha shule ya msingi, miaka 4 ya Shule ya upili na minne chuo kikuu

Mfumo huo aidha uliwapa wanafunzi ujuzi wa umilisi katika masomo kama vile sanaa, kilimo, sayansi ya nyumbani, masomo ya biashara kama njia mojawapo ya kuwatayarisha kwa ajili ya kujitegemea na ujasiriamali.

Na tangia mfumo wa 8-4-4 uzinduliwe mnamo Januari mwaka wa 1985, zaidi ya wanafunzi milioni 26 katika makundi 39 tofauti wamewahi kufanya mtihani wa KCPE, huku pia ukishuhudia wanafunzi wa kigeni kutoka taifa la Sudan Kusini kushiriki kufanya mtihani huo katika mwaka wa 2004 na 2005.
Katika mwaka huu Watahiniwa laki moja nukta tatu wasio raia wa Kenya pia wamefanya mtihani huo wa kitaifa chini ya mtaala wa 8-4-4 kwa hiari yao.

Akisifia mtaala wa 8-4-4 na Mtihani wa KCPE tangu uzinduzi wake Waziri Ezekiel Machogu aliutaja Mtihani huo kuwa wenye mafanikio na kwamba utaacha historia na gumzo la kukumbukwa kwa muda mrefu.

Tangu kuanza kwa mtihani wa 1985 waziri wa Elimu wa zamani Peter Oroa Ringo asingedhania kuwa historia ya safari ya KCPE ingedumu kwa muda mrefu hivi. Na baada ya 1986 kila Waziri wa elimu alisimama hapa kueleza historia ya mafanikio ya Mtihani wa KCPE, historia ambayo itaenziwa na kuelezwa na Wakenya wengi ambao ni wanachama wa mfumo wa elimu ya 8-4-4.” Alisema

Waziri Machogu aliyasema hayo mnamo Alhamisi Novemba 23 wakati wa kutangaza matokeo ya KCPE 2023. Baadhi ya mawaziri waliohudumu chini ya mfumo wa 8-4-4 ni pamoja na marehemu George Saitoti, Mutula Kilonzo, Prof George Magoha, , Jacon Kaimenyi , Dr Fred Matiang Balozi Amina Mohammed na waziri wa sasa Ezekiel Machogu miongoni mwa wengine.

Huku mtihani wa KCPE wa 2023 ukiwa ndio wa mwisho wa katika mfumo huo, mfumo wa 844 unaupisha mtaala wa umilisi wa CBC ambao unatekelezwa nchini kwa sasa.

Kwa kweli, imekuwa safari ya usambamba na usambamba wa safari yenye heri, na changamoto kwa walimu, wanafunzi , wazazi na pia washikadau wote wa elimu nchini chini ya mfumo wa elimu wa 8-4-4 ila sasa pazia lake limefungwa RASMI kupisha KEPSEA.

Kutoka hapa Sauti ya PWANI FM tunasema kwaheri KCPE, karibu KEPSEA.

BY EDITORIAL