HabariMombasaNews

Shule Binafsi Zatamba na Matokeo Bora ya KCPE 2023, Mombasa

Shule za kibinafsi zimeshikilia bendera ya masomo kaunti ya Mombasa kwa kuandikisha matokeo bora katika mtihani wa kitaifa wa KCPE 2023.

Kaunti ya Mombasa, Light Academy Nyali iliandikisha rekodi hiyo kwa kutoa mwanafunzi bora ukanda wa Pwani Khadija Eunice Ahmed ambaye amejizolea alama 426.

Huko shule ya Sheikh Zayed Children imeorodhesha wanafunzi saba waliojizolea alama 400 na zaidi ambapo Hannan Feisal alijipatia alama 407 akifuatiwa na Leyla Salim kwa maksi 406, naye Faiza Abdi Jaber akiwa na maksi 406 huku mvulana Ahmad Alamin akijitokeza kutoana jasho na wasichana hao kwa kuzoa alama 406.

Na katika shule ya msingi ya Memon mjini Mombasa, FATMA ALI ameibuka wa kwanza kwa alama 406 huku wanafunzi watano zaidi wa shule hiyo wakipata alama ya mia nne na zaidi mtawalia.

Mwalimu mkuu wa shule ya Memon, Joseph Ndoro alieleza kuridhishwa na matokeo

Mwaka jana tulikuwa na alama ya wastani 328 lakini sasa tuna alama 335 ambapo tumeongeza alama 7 na tumefurahi sana matokeo haya kwa sababu wanafunzi wamefanya vyema hasa somo la hisabati tuna wanafunzi 15 wamepata alama 90 kwenda juu.” Alisema Ndoro.

Katika shule ya Busy Bee licha ya matarajio yao kama shule hayakuafikiwa walieleza imani kwamba wanafunzi wao walijitahidi na wamejipanga kwa hatua nyingine ya masomo ya sekondari.

Katika shule hiyo wanafunzi wawili pekee walipata alama 400 na zaidi.

Huko kaunti ya Kwale, mwanafunzi Brighton Obara Jared wa shule ya Bethany Academy aliongoza kwa alama 413 akifuatiwa na Juney Pal Mumo mwenye alama 410 naye Zainab Ismail Dosho wa shule ya Mekaela Academy akijizolea alama 405 akifuatiwa na Sophia Shaffie mwenye alama 403.


Takwimu hizo zote kwa jumla Pwani zikiwapa wasichana Khadija Eunice Ahmed wa Light Academy na Hannan Feisal kutoka Sheikh Zayed Children fursa ya kuipeperusha bendera ya wanafunzi bora wa kike Ukanda wa Pwani na kuwapiku wanafunzi wa kiume.

Kwa upande wao wanafunzi walieleza kufurahishwa na matokeo hayo na kutaja nia yao ya kuendelea na masomo ya shule ya upili katika shule walizokuwa wamepanga japo baadhi yao wamesema kwamba walitarajia kupata alama zaidi.
“Naitwa Pamela Athman nimepata alama 401 sikutarajia hili lakini nashukuru natamani kuenda Shule ya upili ya Memon.” Alisema mwanafunzi mmoja.

Mwanafunzi bora kitaifa Michael Warutere aliyepata alama 428 ametokea katika shule ya kibinafsi ya Riara Springs Nairobi.

BY EDITORIAL