HabariLifestyleSiasa

Seneta Omtatah adai maisha yake yahatarini kufuatia kauli ya Rais kukabiliana na wanaopinga na sera zake

Seneta wa Busia Okiya Omtata amedai kuwa maisha yake yamo hatarini kutokana na kauli ya Rais William Ruto kusema atawakabili matapeli ambao wamekuwa wakiwasilisha kesi mahakamani kupinga sera zake.

Haya yamejiri baada ya Rais William Ruto siku ya Jumamosi kusema atawakabili matapeli ambao wamekuwa wakiwasilisha kesi mahakamani kupinga sera zake alipokuwa katika shule ya upili ya wavulana ya Cardinal Otungo Mosocho.

Seneta huyo alidai kuwa kauli hiyo ilikuwa imemlenga yeye na wenzake huku akidokeza kuwa awali alikuwa amepiga ripoti katika kituo cha polisi cha Mosocho alipoelekezwa kurekodi taarifa katika kituo cha Nyanjo.

“Wakati rais alikuwa mosocho siku ile nyingine, alitoa vitisho vya kifo kwa baadhi ya watu mimi nikiwa mmoja wao. Binafsi niko makini sana kuhusu hilo na nishaandikisha taarifa katika kituo cha polisi cha mosocho na nimekuja hapa mahakani kuwasilisha shtaka langu.” Alisema.

Omtatah alidai kuwa OCPD wa kituo alichofika kuwasilisha shtaka na kaundimisha taarifa alimkatalia akidai madai yake hayakuwa na msingi kuwa katiba haikumruhusu kufanya hivyo.

“OCPD amesema kesi yangu haina msingi kikatiba. Ninachofahamu ni kuwa rais amezuiwa dhidi ya kufikishwa mahakamani lakini sheria haijazuia taarifa kuandikishwa dhidi ya rais katika kituo cha polisi na sitaachia hapa nitaendelea…

Ninacholenga ni kuandikisha taarifa kuhusu matamshi ya kikatili na rekodi ambayo itatumika kumchunguza rais baadae akitoka mamalakani. Hicho ndicho nataka mimi.” Alisema.

Kulingana na Omtatah Sheria haimzuii Mkenya yeyote kuandikisha taarifa dhidi ya rais katika kituo cha polisi lakini analindwa na Katiba dhidi ya kushtakiwa na kufikishwa kortini.

Omtatah amesema kauli yake rais ni tishio kwa maisha yake na kwamba rais hana mamlaka ya kumtishia mtu yeyote bali anapswa kuhudumu kwa mujibu wa sheria na katiba ya nchi.

“Hawezi akaniita mkora. Hawezi sema atanikafyeka  mimi na wale wengine kutumia kitara.Hivyo ni vitisho. Rais hana mamlaka kama hayo.Sisi tulienda mahakani kupinga baadhi ya hizi sera za serikali.Tulifaulu na sasa amekasirikia. Anataka kuzuia watu kutopinga sera zake.

Kwani anataka nini? Amesema hawezi kusimamishwa. Njia pekee ambayo hawezi simamishwa ni iwapo ataongoza kwa kufuata sheria. Akiongoza kwa kutofuata sheria, atasimamishwa!” alisema.

BY NEWSDESK