AfyaHabariLifestyleNews

Afueni! Zaidi ya Madaktari 100 kupandishwa vyeo Kaunti ya Kilifi, huku mgomo ukisitishwa

Serikali ya kaunti ya Kilifi imekubaliana na muungano wa madaktari kusitisha mgomo wa madaktari uliokuwa umepangwa kuanzia leo.

Gavana wa kaunti hiyo Gideon Mung’aro ameongoza mkutano wa viongozi wa madaktari hao ambapo makubaliano yameafikiwa kuwapandisha vyeo madakatari 101 na pia kuwapa mikopo ya gari na nyumba.

Aidha Munga’aro amesema kuwa kutokuwepo kwa bodi ya uajiri ndiko kulisababisha kucheleweshwa kwa kupandishwa vyeo madaktari na wafanyikazi wengine.

“Suala tata lilokuwa likipiganiwa ni kuhusu upandishwaji vyeo kwa makundi ya madaktari hawa, maafisa waliokuwa katika Kundi la Kazi J-G sasa wamepanda ngazi hadi Kundi M, na kutoka M hadi N, kisha tuna madaktari 96 waliopanda kutoka kundi N hadi P, na P hadi kundi Q la ajira,” alisema.

Wakiongozwa na mwenyekiti wa Muungano wa Madaktari tawi la Kilifi Kimanga Gichana, madakatari hao wamempongeza gavana huyo kwa hatua hiyo, huku wakiwahakikishia madaktari kuwa mazungumzo yao yalileta natija kwao.

“Kuna mengi tumejadiliana yote katika mfumo huu wa kurejea kazini tunaita ‘return to work formula’ kwa madaktari wetu tunawasihi kuwa tumeelewana mambo yote tumejadiliana, na hukana pahali kuna daktari ameumia katika hii,” alisema.

Madaktari hao pia walihimiza magavana wa kaunti za Tana River na Lamu kuboresha maslahi ya madkatari katika kaunti hizo.

MJOMBA RASHID