Ni afueni kwa wafanyabiashara wodogo Kaunti ya Mombasa baada ya serikali ya kaunti hiyo kutangaza msamaha wa ada na riba ya miaka miwili iliyopita.
Akizungumza na wanahabari afisini mwake mnamo Jumatano, Gavana Abdulswamad Sharriff Nassir alisema hatua hiyo inapania kuwarahishia wafanyabiashara hao kutekeleza wajibu wao ipasavyo ikizingatiwa kuwa gharama ya maisha inazidi kuwakeketa wengi nchini.
Nassir alionya kuwa endapo wafanyabiashara hao hawatalipa sehemu ya madeni hayo ifikapo tarehe 30 mwezi huu wa januari basi serikali yake haitachelea kuwachukulia hatua za kisheria.
“Tunajua uchumi ni mbaya,tunajua hali ni ngumu ndio sababu nimepeana amri zile arreas zote za single business permit ya riba na penalties ziwezekuondolewa.kwa wale ambao hawakuweza kulipa mwaka jana ili wasiweze kuumia wakiwa wanataka kulipa mwakahuu,nimepeana amri kuanzia sasa mpaka mwisho wa mwezi wale ambao hawakulipa mwaka jana na juzi waweze kujaribu kupunguza deni lao.”Alisema Gavana Nassir.
Aidha gavana huyo amewataka wafanyabishara ambao hawajasajili biashara zao kuzisajili kabla mwishoni mwa mwezi huu akisema kuwa serikali yake imeunda jopokazi maalum kitakachozikagua biashara ambazo hazijasajiliwa pamoja na kuwatambua waliokaidi ulipaji ushuru.
Pia amewahimiza wafanyabishara kuwajibika vilivyo katika ulipaji ada ili kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo katika kaunti hiyo.
“Kuna wengi ambao tumefanya mapping wanafanya biashara,wengine walikuwa bado hawajisajili,tumepeana teams ambazo zitahakikisha ya kuwa wale ambao wanalile deni waweze kuzungumza nao kwa uzuri lakini ikifika mwisho wa mwezi then the enforcement team is the one then will now be on the ground.” Aliongeza Nassir.
BY BEBI SHEMAWIA