HabariNews

Ruto akiwasha tena! Asisitiza Kuwang’oa maafisa fisadi wa Mahakama

Kwa mara nyingine tena rais William Ruto ameapa kukabiliana na maafisa fisadi katika idara ya mahakama anaodai wanahujumu mipango na sera za Serikali.

Katika taarifa yake mnamo siku ya Alhamisi kwenye mtandao wa X (zamani ikijulikana twitter) Ruto alisema kuwa hatasita katika juhudi za kupambana na maafisa hao.

Katika kile kimeonekana kama kuwajibu moja kwa moja mawakili tajika Ahmednasir Abdullahi na Paul Mwite katika mtandao huo, Rais alisisistiza kuwa yuko kwenye harakati za kuwang’oa maafisa hao fisadi katika idara hiyo.

Kauli ya rais inajiri wakati kuna mjadala mkali unaozidi kutokota kati ya afisi yake na Idara ya Mahakama huku vuta nikuvute ikizidi kushuhudiwa.

Haya yanajiri baada ya Rais William Ruto kusema kwamba baadhi ya maafisa katika idara ya mahakama wamekuwa wakitatiza na kulemaza ajenda ya serikali yake kwa kupiga marufuku utekelezwaji wa miradi muhimu kama vile mradi wa huduma ya afya kwa wote na ujenzi wa nyumba.

 “Ati watu wachache, wawili watatu wameenda kortini, wakahongana kortini mipango hiyo ikasimamishwa…barabara ikasimamishwa, Universal Health Coverage ikasimamishwa, mambo ya housing inasimamishwa…lazima tuulizane, lazima tuwe na mjadala,” Alisema.

Hata hivyo, madai ya Rais yalipingwa na jaji mkuu Martha Koome aliyeyataja kama ya udhalilishaji huku akimtaka rais William Ruto Kufuata taratibu zinazofaa kuwasilisha malalamishi yake kwa tume ya huduma za mahakama JSC iwapo ana ushahidi wowote wa ulaji rushwa na afisa yeyote wa mahakama.

Mnamo siku ya Jumatano, Jaji Mkuu alivunja ukimya wake kwa kuungana na maafisa wengine wa idara ya mahakama kupinga shutma zilizoelekezewa idara hiyo na rais Ruto.

Aliyataja matamshi ya rais Ruto kuwa tishio kwa uhuru wa idara hiyo na kuwa ishara ya uongoizi wa kiimla, huku chama cha wanasheria nchini LSK nacho kikipanga maandamano ya wiki nzima kuanzia wiki ijayo kupinga hatua ya rais kuishambulia idara ya mahakama.

Koome alisisitiza njia sahihi ya kupinga uamuzi wa korti iwapo mtu yeyote hakuridhika na uamuzi ni kupitia kukata rufaa au kupitia mahakama ya upeo.

Kuwashambulia majaji na maafisa wa mahakama waliotoa uamuzi hadharani kunadhoofisha maadili ya utaratibu wetu wa kikatiba.” Alisema Jaji Mkuu.

Itakumbukwa kuwa mnamo siku ya Jumanne rais William Ruto akiwa huko kaunti ya Nyandarua alitishia kukiuka uamuzi wa mahakama akitaja majaji kuwa mafisadi.

Idara yetu ya Mahakama, tunawaheshimu lakini ulaghai wa mahakamani unaofanywa na maafisa fisadi lazima usitishwe…Tutawazuia liwe liwalo,” alisema rais Ruto.

Koome alitaka madai yoyote ya utovu wa nidhamu au vitendo vya ufisadi vya majaji au maafisa wowote wa mahakama kuelekezwa kwa tume ya Huduma za Mahakama JSC kwa hatua mwafaka za haraka kuchukuliwa.

Licha ya Jaji Mkuu huyo kudokeza kuwa atatafuta kikao na Rais na Bunge ili kutatua utata na tofauti zinazoendelea kurindima.

Je, kauli yake rais inaashiria nini katika mzozo huu unaoendelea kutokota?

BY NEWSDESK