HabariNews

Nimekubali na ni Tayari kwa Mazungumzo na Mahakama kukabili Ufisadi; Rais Ruto asalim amri

Rais William Ruto amesema kuwa yu tayari kukutana na uongozi wa Idara ya mahakama chini ya Jaji mkuu Martha Koome, ili kushughulikia suala la ufisadi.

Rais amebaini kuwa atafanya hivyo kwa kuendeleza ushirikiano kati ya Serikali Kuu, Bunge na Idara hiyo ya Mahakama kukabiliana na Donda hilo sugu nchini.

Akizungumza huko Tinderet katika kaunti ya Nandi, Rais amesema viongozi wa idara zote za serikali wanafaa kuwa na kikao kujadili kwa kina suala la rushwa ambalo limekuwa kikwazo kwa kuchelewesha utekelezwaji wa miradi ya serikali.

“Mimi nimekubali yale madam Chief Justice alisema kwamba tukutane, kama rais niko tayari kukutana na viongozi wa Mahakama, kukutana na viongozi wa Bunge na sisi kama Serikali Kuu ili tuondoe mamabo ya ufisadi na mambo yale mengine ambayo yanakwamisha maendeleo ya taifa letu la Kenya,” alisema.

Kwa mujibu wa Rais uongozi mbaya na ufisadi ndio umelemaza ukuaji wa miradi muhimu ya serikali na jukumu lao kama viongozi ni kutafuta suluhu la kudumu kwa tatizo hilo.

“Maendeleo ya Kenya imekwama kwa siku nyingi na imekwamishwa na uzembe katika uongozi na imekwamisha na watu ambao wameteka nyara nchi yetu na ni watu wachache na watu fisadi,” alisema.

Kiongozi wa Nchi alisisitiza dhamira ya Serikali ya kutetea uhuru wa Mahakama.

Hata hivyo, alisema Serikali itakabiliana vilivyo na rushwa katika Mahakama ili kurejesha uaminifu wake.

 “Tuna watu wengi katika Mahakama wenye uadilifu. Ndio maana lazima tukabiliane na wale wanaotaka kuharibu uaminifu wa mfumo wetu wa mahakama,” akasema.

Itakumbukwa kuwa haya yanajiri siku moja baada ya Jaji Mkuu Martha Koome mnamo siku Jumatatu kuonya kuwa huenda nchi ikatumbukia katika mgogoro mkubwa wa katiba hali itakayopelekea ghasia na machafuko iwapo utawala wa Kenya Kwanza utazidi kupuuza maagizo ya mahakama.

“Vitisho hivi na kauli za viongozi wakuu serikalini za kutoheshimu maagizo ya mahakama inatishia sana uthabiti wa taifa hili na kuhujumu katiba yetu. Ni hujuma kwa utawala wa sheria nchini na inaweza kupelekea machafuko na mgogoro nchini mwetu,” alisema.

Awali Jaji huyo Mkuu alikuwa ametoa mwanya wa kumwalika rais kukutana na maafisa wa idara hiyo kujadili masuala yanayoleta mvutano na mzozo.

BY MJOMBA RASHID