HabariNews

Washukiwa wa Mauaji ya Shakahola Kuzuiliwa kwa Siku 14 Zaidi

Mahakama kuu mjini Malindi imetoa siku 14 zaidi Kwa idara ya upelelezi kuendelea kuwazuilia washukiwa 31 wanaohusishwa na mauaji ya Shakahola.

Akitoa uamuzi huo Jaji Mugure Thande alisema muda huo unatosha kuwafanyia vipimo vya akili washukiwa wote akiagiza idara ya mashtaka ya umma kuhakikisha kila mshukiwa anapata wakili kabla ya kushtakiwa na kosa la mauwaji.

Awali mawakili wa washukiwa hao Wycliff Makasembo na James Mouko walipinga ombi hilo la upande wa mashtaka kuendelea kuwazuilia washukiwa wakisema haki za washukiwa zinakiukwa.

Makasembo aliwatetea wateja wake akisema usimamizi wa gereza la Shimo la Tewa umekuwa ukiwanyima chakula akiitaka Mahakama kutoa amri Kwa usimamizi huo kukoma kufanya hivyo.

Aidha upande wa Mashtaka ukiongizwa na Naibu Mkurugenzi wa Idara hiyo Victor Mule ulilitetea ombi hilo ukisema washukiwa hawawezi kusomewa mashtaka kisheria kabla ya kupimwa akili.

Jaji Mugure hata hivyo aliamuru washukiwa hao kufikishwa tena mahakamani Februari 6 ili wasomewe mashtaka.

 

BY JOSPH YERI