HabariNews

Aombe Msamaha! Viongozi Kwale wamkashifu Odinga kudai Gavana Achani ni Mke wa Waziri Mvurya

Gavana wa Kaunti ya Kwale Fatuma Achani ametoa makataa ya siku 7 kwa kiongozi wa ODM Raila Odinga kuomba msamaha Kwa matamshi aliyoyatoa jana kwenye usajili wa wanachama wake.

Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari kutoka afisi yake ya mawasiliano Achani amesema kuwa matamshi ya kiongozi huyu ni moja kati ya dhulma za kijinsia na pia kuhujumu juhudi za wanawake kuwania viti vya uongozi.

Gavana huyo hata hivyo alipata uungwaji mkono kutoka kwa viongozi wa matabaka mbalimbali pamoja na wakaazi waliomshtumu Kinara huyo wa ODM kwa kumharibia jina Gavana Achani na kumtaja mwenye nia ya kutaka kukandamiza mwanamke katika nafasi ya uongozi.

Matamshi yake Raila ni hujuma kwa gavana wetu, ni matusi na kejelialitunyanyasa sisi wanawake na kutudhulumu, kwa nini azungumze vile akiwa Kwale? Ametuumiza na tunasikia uchungu, hivi mume wake Achani unajua amejiskiaje? Kama ni uchochezi sio vizuri Raila Odinga aache na akome.” Alisema mmoja wa wakazi hao, Binti Hassan

 

Kwa upande wao viongozi wa kidini wakiongoza na Mchungaji Esther Ngugi na Sheikh Amani Mwachirumu wamekashifu vikali kiongozi huyo wa upinzani wakisema kuwa kulingana na sheria ya kidini ndoa ina hadhi yake na  inafaa iheshimiwe kivyovyote.

“Tukiwa viongozi wa Kidini wa Kwale tunatoa siku 14 kwa Raila Odinga atoe msamaha kwa mama Achani,” Alisema Sheikh Mwachirumu.

 

“Tunamshauri Raila afanye siasa zake na kuheshimu mambo ya ndoa za watu wengine hasa viongozi, ndoa ya mama Achani inamhusu nini na siasa za ODM, Si vyema kabisa na tunakemea hilo.” Alisema Mchungaj, Bi. Ngugi.

Mohammed Mwakisuwa mmoja wa wanafamilia walimtaka Odinga kuomba Msamaha la sivyo wachukue hatua za kisheria.

“Odinga ulimwambia Isa Juma Boi kwa nini unatembea na Achani nay eye ni mke wa Mvurya, vipi Achani ni mke wa Mvurya na tunajua mke wa Mvurya ni mama Christine Mvurya na Achani shemeji yangu mume wake ni Ali Kanga, tunashanga kwa hii tuhuma mbaya tunashangaa ukisema hivyo tunataka utupe ushahidi, bila ushahidi tutachukua sharia za kinidhamu kwa sababu ndoa si siasa.” alisema.

Haya yanajiri siku moja baada ya Kinara wa ODM Raila Odinga mnamo siku ya Alhamisi akiwa katika mkutano wa hadhara wa kusajili wanachama wapya wa ODM huko Kwale, Kuzungumzia uhusiano wa kimapenzi baina ya Gavana huyo na Waziri wa Madini Salim Mvurya.

Akimzungumzia Seneta Isa Boi Odinga alisema, “Nasikia umelemea pande ile sana huyu mama umemkalia yeye sana na unajua huyu ni bibi ya Mvurya.”

Kinara anaendeleza ziara yake ukanda wa Pwani na siku ya Ijumaa alikuwa kaunti ya Taita Taveta kuongoza zoezi la usajili wa wanachama wa ODM ili kukiiimarisha na kuongeza ufuasi wake eneo la Pwani likiwa ngome yake kuu.

BY BINTIKHAMIS MOHAMMED