HabariNews

Wakereketwa wa maswala ya ubaharia wazungumza

Wakereketwa wa maswala ya ubaharia kaunti ya Mombasa wamesema ipo haja ya serikali ya kaunti hiyo kujizatiti zaidi kutoa mafunzo kwa vijana kuhusiana na maswala ya uchumi samawati.

Wakiongozwa na Albert Adembesa wakereketwa hao walisema kaunti ya Mombasa iko nyuma katika kutoa mafunzo ikilinganishwa na kaunti nyingine za Kwale na Kilifi.

Aidha Adembesa aliongeza kuwa viongozi kwenye sekta hiyo hawajajukumika vilivyo kuhakikisha vijana wengi wanahusishwa katika maswala ya uchumi samawati kama njia moja ya kuweka nafasi za kazi.

“Kaunti zingine tumeziona zikisomeshwa katika mfuko wa kaunti lakini kaunti yetu ya Mombasa imekuwa nyuma maanake ukiuliza kaunti ya Mombasa imesomesha watu wangapi hatuoni na kazi hizi zinakuja hapa Mombasa na hatujaona kaunti ikiwekeza katika maswala haya basi tunaamini kwamba watu watatoka sehemu nyingine kuchukua zile kazi.” Alisema Adembesa.

Wakati huo huo Adembesa ameongeza kuwa kunahaja ya kuwepo na viongozi watakao kuwa na ufahamu kuhusu sekta hiyo na kushirikiana na wataalamu ili kutoa mafunzo kwa jamii  hali ambayo ameitaja kustawisha uchumi wa Mombasa.

 

“Tunaamini kwamba kama tunataka mabadiliko katika kaunti ya  Mombasa ni vizuri tusomeshe watu wetu ili waweze kunufaika katika maswala ya ubaharia lakini kama kaunti haina ujumbe kama huu haiwezi kuendelea katika maswala haya na tunaamini kwamba lazima kuwe na waziri katika kaunti anayefahamu uchumi samawati ni nini na umuhimu wake na pia faida yake.”Alisema Adembesa

BY NEWS DESK