AfyaHabariLifestyleMazingiraMombasaNews

Walanguzi sugu wa mihadarati Wanaswa Mtwapa, kaunti ya Kilifi

Mamlaka ya Kitaifa ya kukabiliana na dawa za kulevya na matumizi ya Pombe, NACADA imewakamata watu wawili huko Mtwapa kaunti ya Kilifi kwa kuhusika na ulanguzi wa mihadarati.

Katika msako mkali dhidi ya walanguzi wa dawa za kulevya ulioendelezwa na NACADA kwa ushirikiano wa maafisa wa polisi eneo la Mtwapa, umepelekea kunaswa kwa watu hao na pia kupatikana misokoto 435 ya bangi inayoaminika kutokea kaunti ya Migori.

Miongoni mwa waliokamatwa ni pamoja na muuzaji bangi maarufu eneo la Pwani ambaye amekuwa katika orodha ya walanguzi sugu wanaosakwa na mshukiwa wa pili pia akitajwa kama mlanguzi sugu anayeunganisha biashara hiyo haramu kati ya mjini Kilifi na Malindi.

Akizungumzia tukio hilo la kunaswa kwa walanguzi hao Afisa Mkuu wa NACADA Dkt. Anthony Omerikwa amefichua kuwa wana vyanzo vya taarifa muhimu kuhusiana na wasambazaji wakuu wa mihadarati na wanawafatilia ili kuwakabili katika siku zijazo.

“Baada ya kuwakamata watu hao wawili tumeweza kupata taarifa kwamba ni kweli mihadarati hii inadaiwa kutokea Migori kaunti. Tuna vyanzo muhimu kuhusu ni nani Wasambazaji wakuu, na tunawafuatilia kwa karibu hivi karibuni tutawanasa,” alisema.

Mkurugenzi huyo aidha amedokeza kuwa msako wa dawa za kulevya umeanza rasmi eneo la Pwani huku wafanyabiashara wadogowadogo wakikamatwa kusaidia uchunguzi wa maafisa, akiwataka wakazi kushirikiana katika kutoa taarifa ili kukabiliana na uozo wa mihadarati eneo hili.

“Huu ni mwanzo na tuko hapa kupambana na vita hii, manoari imeng’oa nanga. Kuna wazee wameninong’onezea mambo kadhaa hapaa, na hii area hatutoki haraka tutafuatilia hawa walanguzi. Na wananchi mtupatia taarifa.” Alisema.

Katika msako huo aidha pikipIki kadhaa zimenaswa wakati oparesheni hiyo.

Haya yanajiri huku ripoti ya NACADA yam waka 2022 kuhsusu mihadarati ilibaini kuwa matumizi ya bangi yameongeza maradufu huku eneo la Pwani likiwa na watumizi wengi kwa ongezeko la asilimia 90.

BY MJOMBA RASHID