Kwa mara nyingine tena Kinara wa Muungano wa Azimio la Umoja Raila Odinga amepuuzilia mbali madai ya kusambaratika kisiasa kwa muungano huo.
Akiongea huko kaunti ya Kitui wakati wa hafla ya mazishi, Odinga alisisitiza kuwa Viongozi wa muungano huo hawajagawanyika na kwamba mustakbali wa kisiasa wa mrengo huo ungali imara licha ya uvumi na madai hayo.
Alisema uvumi na madai ya kubadilishwa kwa mgombea atakayepeperusha bendera ya muungano huo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 si ishara ya kugawanyika kwa viongozi, akidokeza kuwa wanaoendeleza uvumi huo wana nia ya kusambaratisha muungano huo.
“Sisi tuko imara na tumeungana, na Tutakubaliana, maana hakuna ubaya, nimetoka mbali pamoja na yeye (Kalonzo) na naweza kumuunga mkono,” alisema Raila.
Hata hivyo kinara huyo alionesha ishara ya kumuunga mkono azma ya Kalonzo kuwa mgombea wa Muungano huo mwaka 2027 akisema kuwa hakuna ubaya wowote iwapo Kalonzo atakuwa mgombea debeni.
“Kila mahali mimi naenda naongea mambo ya Azimio ooh imegawanyika… lakini sisi tuko pamoja ati ooh Kalonzo anatangaza anasimama na baba namna gani ati mpaka baba asimame. Hapana…kama Kalonzo ni candidate kuna ubaya gani?” aliashiria Raila, huku wananchi wakimshangilia.
Hata hivyo Viongozi wa Azimio walisema wanaendelea kushirikiana kupigania haki za Wakenya huku akibaini kuwa muungano huo unaendeleza mikakati na mazungumzo ya ni nani atakayechukua uongozi wa muungano huo kabla ya muda wa uchaguzi mwingine kufika akiwataka wananchi kuwa na subira.
Eugine Wamalwa kiongozi wa chama cha DAP-Kenya ambacho ni chama tanzu katika Azimio alisisitiza kuwa chama hicho kingali imara na kwa umoja.
“Kwa wale ambao wanaweka madai kwamba Azimio imegawanyika, nataka kuwahakikishia Azimio inasalia kuwa pamoja, imara zaidi na yenye malengo kupigania Wakenya kuwaondolea mateso ya ‘Zakayo’ na ushuru wake,” alisema.
BY MJOMBA RASHID