HabariLifestyleMakalaMombasaNewsSiasa

Hakuna Ukatili wa Polisi na Utumizi wa Nguvu nchini Kenya, asema Mudavadi

Visa vya ukatili wa polisi na utumizi wa nguvu kupita kiasi havijaripotiwa hapa nchini Kenya. Ni kauli yake Waziri mwenye mamlaka Makuu na masuala ya kigeni, Musalia Mudavadi.

Akijibu tuhuma za Tume ya Afrika kuhusu haki za kibinadamu Mudavadi ametetea rekodi ya haki za binadamu nchini na maadili ya idara ya huduma za polisi.

Mudavadi amesema visa vya dhulma na ukandamizaji wa polisi havijawahi kuripotiwa na badala yake amebaini kuwa Wakenya wapo huru kuripoti visa vyovyote vya dhulma na unyanyasaji wa polisi bila hofu kwa Mamlaka ya Kutathmini Utendakazi wa Polisi, IPOA.

Mudavadi ambaye anahudhuria mkutano wa 44 wa Muungano wa Afrika, AU kuhusu masuala ya Kigeni jijini Addis Ababa nchini Ethiopia amesema IPOA imepewa mamlaka ya kutosha kuwawajibisha maafisa wa polisi wanaowanyanyasa wananchi.

Akipongeza juhudi za Tume hiyo ya Afrika katika kulinda haki za Waafrika, Mudavadi amesema kuwa taifa la Kenya litaendelea kuzingatia mwongozo wake kuhusu haki za kibinadamu na kusitisha ukosefu wa utaifa na kubadili hukumu ya kifo kuwa kifungo cha maisha.

BY MJOMBA RASHID