HabariMombasaNews

Serikali Ibuni Nafasi zaidi za Ajira za Ndani ya Nchi na Si Ughaibuni

Serikali inahimizwa kubuni nafasi zaidi za ajira kwa vijana hapa nchini badala ya nchi za ughaibuni.

Akizungumza na Sauti ya Pwani mnamo Alhamisi, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la vijana Stretchers Dickson Okong’o alisema kazi za nje ya nchi zina mahitaji mengi yakiwemo kupata stakabadhi muhimu za usafiri pamoja na visa vya kufanyia kazi.

Okong’o amesema swala la ukosefu wa ajira si jambo geni nchini na hata kimataifa bali ni tatizo la ulimwengu mzima hivyo kuna haja nafasi zaidi za ajira zikabuniwa ndani ya nchi.

Rais amesema kuna kazi nje na tunajua ukosefu wa kazi si jambo la Kenya pekee ni jambo la Ulimwengu mzima lakini kwangu mimi naeza sema ni vizuri tuwe na zile nafasi za kazi, lakini kwa nini zisitengenezwe hapa nchini kuliko kwenda nje kutafuta nafasi za ajira.” Alihoji.

Okong’o aliongeza kuwa kubuni nafasi za ajira humu nchini kutaimarisha uchumi wa nchi huku akibainisha kuwa serikali inafaa kuangazia sekta ya mazingira ili kubuni nafasi za ajira na pia kuwakaribisha wawekezaji humu nchini bila kuwatoza ushuru ya hali ya juu.

Vile vile aliesisitiza kuwa serikali inafaa kuwasaidia vijana katika biashara zao ili kuwaonyesha kuwa serikali inawapongeza kwa bidii yao huku akitoa mfano wa kampuni ya EPZ kuwa na uwezo wa kuajiri vijana 3000.

“serikali itengeneze mazingira mazuri ya kufungua kazi na mazingira mazuri ni kama kuwakaribisha wawekezaji na tusiwatoze ushuru ya juu sana na tuwasaidie vijana wanaofanya kazi ili wahisi ni kama wanashukuriwa kwa mfano kampuni ya EPZ ambayo inaweza kuajiri watu zaidi ya elfu 3000.”

Kauli yake imejiri siku moja baada ya rais William Ruto kusema kuna nafasi milioni moja za ajira katika mataifa ya ughaibuni, nafasi ambazo zilijitokeza kupitia mikataba mbalimbali aliyosaini kwenye ziara zake za nje ya nchi.

BY NEWSDESK