HabariLifestyleMombasaNews

Chakula cha Msaada Mwezi wa Ramadhan Chazua Mihemko Mombasa.

Viongozi wa dini ya kiislamu katika kaunti ya Mombasa wameikashifu Serikali kuu Kwa kile wanachodai ni kubadilisha mkondo na utaratibu wa ugavi wa chakula cha msaada cha mwezi mtukufu wa Ramadhan kwa waumini wote wasiojiweza katika kaunti ya Mombasa.

Katika kikao na waandishi wa habari,mnamo Jumatano viongozi hao kutoka Baraza kuu la Waislamu la SUPKEM pamoja na Baraza la Maimamu na Wahubiri nchini CIPK, waliisuta vikali hatua ya serikali kuu kukabidhi jukumu la ugavi wa chakula hicho kwa wanasiasa kinyume na desteuri na utaratibu wa hapo awali ambapo zoezi hilo limekuwa likiendeshwa na viongozi wa kidini kila mwaka.

Mwenyekiti wa SUPKEM Athman Ali alisema kuwa hatua ya kubadili mkondo na utaratibu uliofuatwa kwa miaka kumi iliyopita, huenda ikakosa kuwafaidi walengwa na hata kuingizwa siasa.

Ali aliongeza kuwa uamuzi wa kuwatwika jukumu hilo Mbunge wa Nyali Mohammed Ali na Seneta Maalum Miraj Abdillahi ambao ni wa mrengo mmoja wa kisiasa sio tu unadhalilisha uongozi wa kidini bali pia huenda una nia fiche.

Mwenyekiti huyo aidha alifichua kuwa juhudi za viongozi wa kidini za kufanya mkutano na kamshina wa kaunti ya Mombasa kujadili suala la hilo kwa kina ziligonga mwamba, baaada ya kamishina huyo kusema kuwa alipewa maagizo kutoka serikali kuu, kauli ambayo kulingana nao inazidi kuibuia maswali chungu nzima wasijue ni kwa nini serikali imechukua mkondo tofauti katika ugavi wa chakula hicho mwaka huu.

“Leo asubui tulikuwa kwa kamshina na alichotwambia hakitufurahisha kwamba amepewa maagizo kutoka juu ya kwamba chakula atapewa Mohammed Ali na Seneta Miraj,hatukujua ni kwa nini wamefata mkondo huo ni vipi leo chakula chapewa wanasiasa tena wa mrengo mmoja hatungekuwa na malalamiko iwapo wangehusisha wabunge wote wa Mombasa lakini mbona Mrengo mmoja.” Alisema Ali

Kwa upande wake Mahmoud Abdillah ambaye ni Katibu wa mipango na uratibu wa baraza la Maimamu kaunti ya mombasa, alisema viongozi wa dini wamekuwa wakiendesha zoezi hilo kwa zaidi ya miaka kumi kwa kuzingatia takwimu za waislamu mashinani hususani wanaohitaji msaada , ila sasa wanaelezea hofu yao kuwa huenda  wanasiasa wakatumia fursa hiyo kujinufaisha hali ambayo itakapelekea msaada huo kukosa kuwafaidi walengwa .

“Sisi tunaambia serikali kuu kwa miaka kumi chakula kinakuja kwa mashirika haya kwa sababu twawajua wale wanahusika, twataka chakula hiki kipewe mashirika kisipewe wanasiasa, na pia tunamuuliza waziri mbona amewapa wanasiasa na miaka yote anawapa viongozi wa dini na mbona ni Mombasa pekee kaunti zingine wameshapewa hata washagawanya.” Alisema Abdillah

Rajab Ismail mwenyekiti SUPKEM eneo la Mvita, aliitaka serikali kupitia kamishna wa kaunti hiyo kuweka wazi utaratibu gani wataufata kugawa chakula hicho akisema kuwa kaunti nyingine viongozi wa kidini wameshirikishwa kikamilifu.

“Serikali watatumia mbinu gani na mfumo gani kutambua wale ambao wahastahili kupata kile chakula,mbona kamshina hajaitisha kikao cha majadiliano jinsi chakula kitagawiwa,tufanye kikao cha dharura ili tuwe na mpangilio mzuri wa kugawa hiki chakula kwa waislamu.” Alisema Ismail.

Kauli za viongozi hao zinajiri huku wengi wakielezea hofu yao iwapo chakula hicho kitagawanywa kisiasa na kukosa kuwafaidi waumini wote wasiojiweza kipindi hiki cha mwezi huu mtukufu wa Ramadhan.

BY ISAIAH MUTHENGI.