HabariNews

Ufunguzi wa Bunge Tower; Rais Asema Bunge Halihitaji tena Pesa kukongamana Hotelini

Hakuna sababu tena ya kuhitajia raslimali zaidi na fedha za ziada kutumika kusafiri kwenda kufanya vikao vya kamati za bunge katika hoteli.

Ni kauli yake Rais William Ruto, akizungumza mnamo Alhamisi Aprili 25, katika hafla ya ufunguzi wa Jengo la Bunge Towers jijini Nairobi.

Rais aliyeongoza ufunguzi huo alisema anatarajia bajeti ya Bunge kupungua kwa kiwango fulani kutokana na kuwa Jumba hilo lina vyumba vya mikutano na vifaa vyote hitajika.

Rais Ruto amelitaka bunge kuzingatia kupunguza gharama ya bajeti yake watakapokadiria mipangilio ya bajeti yake ijayo ya mwaka wa kifedha.

Hakuna sababu tena sasa kuhitajika kwa raslimali za ziada kusafiri kwa mahoteli na hadi sehemu zingine (sijui kama ni kweli) tukiwa na vifaa vyote hapa, vymba vya mikutano, vyumba vya kamati kukutana ninatarajia kupungua kiasi cha haja bajeti yenu Bwana Spika…” alisema.

Lazima ifikie mahali, nyinyi mmesema wenyewe hapa… hivyo mkikadiria bajeti ijayo, mkumbuke kuwa Bunge sasa halihitaji pesa kwenda hotelini na hivyo bajeti itashuka chini.” Alisema Rais

Wakati uo huo Rais alieleza matumaini yake kuwa wabunge watajizatiti vilivyo katika utendakazi wao huku akisisitiza kuwa ni lazima bunge lifanye kazi kwa ushirikiano na Serikali Kuu kukabiliana changamoto za kimaendeleo ili kuwahudumia wakenya.

Nina imani kila mbunge atajitahidi vilivyo na amejitolea na anaweza kufanikisha maendeleo zaidi ya inavyotarajiwa, niwatakie mafanikio katika kulitumikia taifa katika ofisi zenu mpya za Bunge Towers na natarajia ushirikiano mzuri na wa dhati katika kufanikisha matarajio ya Wakenya na kuzikabilia changamoto. Alisema.

Jumba hilo la Bunge Towers la ghorofa 28 lililogharimu shilingi bilioni 9.6 lina afisi 331 za wabunge ambapo wabunge wataanza rasmi kutumia ofisi hizo, lina pia migahawa na vilabu vya afya.

Jumba hilo lilichukua miaka 14 kukamilika na lilifunguliwa Alhamisi katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo, Naibu Rais Rigathi Gachagua, Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, Maspika wa Bunge la Kitaifa na Seneti na wabunge.

BY MJOMBA RASHID