Ulimwengu ukihamisha shughuli zake nyingi kwenye mtandao, wito umetolewa kwa wafanyabiashara wadogo kupata ujuzi wa kujikinga dhidi ya udukuzi wa mitandao wanayofanyia biashara zao.
Andrew Sikudhani mwasisi wa kampuni ya Merime Space ameeleza kuwa mafunzo hayo kuhusu hatari ya kudukuliwa kwa mtandao yatawasaidia wafanyabiashara hao kuepuka hasara kutoka kwa walaghai hasa wanapotangaza biashara zao kupitia mitandao.
“Ni muhimu kwamba tuwe na ufahamu kuwa tuko wakati ambao udukuzi uko kwa viwango vya juu. Na nadhani wafanyabiashara wengi wanafikiria kwamba ni wadogo sana hawawezi kudukuliwa lakini ukweli ni kwamba hakuna mtu ambaye ni mdogo kwa udukuzi.
“Na hakuna mtu ambaye anapopata changamoto ya kudukuliwa hatapata madhara, kwasababu kila udukuzi una madhara yake. Unaweza kuwa kwako moja kwa moja kwa biashara yako ama labda hata barua pepe yako imedukuliwa na wateja wanaanza kutumiwa bila ufahamu wako na unaweza kupoteza hata pesa.” alisema Sikudhani.
Ephie Chari Wesa mfanyabiashara mjini Kilifi amesistizia haja ya hamasa ya mara kwa mara kutolewa ili kuwaepusha wafanyabiashara kulaghaiwa huku akiongeza kuwa ulaghai wa mitandaoni umekuwa ukiongezeka kila uchao.
“Kwa hivyo leo ni kitu ambacho nimefundishwa na nahisi ni muhimu kwa kina mama wote, vijana wote, na wale wote walio kwenye mitandao kila siku haya ni mafunzo ambayo ni muhimu. “Na hata nitaanza na hapa nyumbani kaunti ya Kilifi kila mmoja iwe una biashara ndogo ama kubwa upewe mafunzo ndio uelewe kwanini tunatumia mitandao vibaya bila kuelewa kuwa itakuwa na madhara siku zijazo.” alisema Bi. Wesa
Hayo yamejiri wakati wa warsha ya kutoa hamasa kwa wafanyabiashara kuhusu udukuzi mitandaoni iliyoandaliwa na mashirika ya GIZ Kenya na GFA kaunti ya Kilifi.
Ikumbukwe mnamo Julai mwaka jana, waziri wa mawasiliano nchini Eliud Owalo alithibitisha kuwapo kwa na jaribio la udukuzu kwenye mfumo wa E Citizen baada ya mfumo huo kuwa na matatizo siku chache katika kutoa huduma muhimu kwa wananchi.
ERICKSON KADZEHA.