Ipo haja wanahabari kuangazia kwa kina taarifa za mabadiliko ya Tabianchi ili kuifahamisha jamii mchango wao na athari zake.
Akizungumza na wanahabari hapa mjini Mombasa kwenye warsha ya mafunzo kuhusiana na mabadiliko hayo Rais wa Baraza la Wahariri nchini (KEG), Zubeida Kananu alisema kumekuwa na pengo kwa wanahabari katika kuangazia taarifa hizo kwa lugha na namna itakayomfikia mwananchi wa kawaida.
Zubeida alibainisha kwamba kutokana na hayo Baraza la Wahariri kwa ushirikiano na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) wanapania kubuni mtaala wenye msamiati utakaotumika kutoa mafunzo kwa wanahabari jinsi ya kuripoti taarifa hizo ili kumfaidi mwananchi kwa wakati mwafaka na kupukana na athari hizo.
“Tutengeneze ile module ambayo tutatumia kuweza kuwafunza wanahabari kuhusu namna ya kutoa taarifa ambazo zinahusiana na mabadiliko ya tabianchi, namna tunavyochangia kama jamii n ani vipi tunaweza kukabili athari ambazo zinatokana na mabadiliko ya tabianchi,” alieleza Zubeda.
Wakati huo huo Zubeida alieleza kuwa kutokana na mabadiliko hayo vyombo vya habari kwa sasa vinapaswa kuwekeza zaidi na kuwa na Idara maalum ya kuangazia taarifa na vipindi kuhusiana na mabadiliko ya tabianchi.
Vile vile akitoa wito wa kuwawezesha na kuwapa nafasi wanahabari wa kike katika kuangazia taarifa za mabadiliko ya tabianchi sawia na taarifa zenye masuala mazito ya kitaifa badala ya kuachiwa wanahabari wa kiume pekee.
“Sasa vyombo vya habari vingi vimeanza kuekeza katika sayansi na masuala kuhusu mabadiliko ya tabianchi. Mambo yameanza kubadilika, ni ile kutoa wito kwa vyombo vya habari kuhakikisha kwamba hata jinsia ya kike haiachwi nyuma katika safari hii,” alisisitiza Zubeda.
BY MJOMBA RASHID