HabariNews

Mahujaj Mjini Makka Waanza rasmi Ibada ya Hijjah, Siku Kuu ya Eid ul Adh-ha Kuadhimishwa Jumapili Juni 16

Kadhi Mkuu nchini Sheikh Abdulhalim Athman amewataka Waumini wa dini ya Kiislamu nchini kuyatumia masiku 10 ya mwezi wa Dhul Hija kuzidisha maombi na ibada.

Amesema siku 10 hizo za mwezi wa 12 kwa mujibu wa kalenda ya Kiislamu zimeanza rasmi leo kwa munasaba wa mahujaji walioko mji mtakatifu wa Makkah, Saudi Arabia.

Amewausia waumini hapa nchini kufunga siku hizo 10 kuanzi leo na kutia nia ya kuchinja katika siku kuu ya Eid ul Adh-ha ili kupata baraka sawia na kufuata kanuni na mafunzo ya dini.

Mahakama Kuu ya Mamlaka Arabiya ya Saudia ilitangaza kuwa Ijumaa tarehe 7 Juni 2024 ndio siku ya kwanza ya mwezi wa Dhul Hajj, tunawaomba waislamu waanze kufunga na asiyeweza kufunga kila siku katika siku hizi 9 basi siku ya Jumamosi tarehe 15 Juni ndio itakuwa kisimamo cha Arafat na hiyo ni siku muhimu kabisa mtu asikose.

Tunawaambia kila mtu atie nia kuchinja na ni sunnah kama utachinja basi uanze kuwacha kujikata kucha na kunyoa nywele mpaka siku ya Eid, kama isemavyo hadithi ya Mtume S.A.W unaweza kufanya hivyo kuifananisha na mahujaji na pia kusisitiza umoja wetu na wale wenzetu walioenda kuhiji.” Alisema Kadhi Mkuu Abdulhalim.

Kadhi Mkuu huyo aidha alitangaza Jumapili ijayo tarehe 16 Juni, 2024 kuwa Siku kuu ya Eid ul Adh-ha, sikukuu ambayo huadhimishwa kila tarehe 10 ya mwezi wa 12 kwa mujibu wa kalenda ya Kiislamu maarufu (Hijriyah).

Siku ya Eid itakuwa Jumapili tarehe 16 Juni, 2024 in sha Allah na tunawatakia Eid njema na amali njema, Mungu awabariki na Kullu a’amun wa antum bikheir.” Alisema.

Katika sikukuu hiyo waumini huchinja kwa kumbukizi ya Mtume Ibrahim (A.S) alipoamrishwa na Mwenyezi Mungu (S.W.T) kumchinja mwanawe Ismail (A.S) kabla ya Mungu kumbadilishia amri hiyo kwa kumtoa Kondoo aliyemchinja kama kafara yake.

Mahujaji wa Kiislamu wameanza ibada rasmi ya Hijjah Ijumaa Juni 7, huko mjini Makkah nchini Saudi Arabia.

Hii ni baada ya kutangaziwa kuandama kwa mwezi na Mamlaka ya Hijjah nchini humo.

Ibada ya Hajj ni ibada muhimu na ya lazima kwa Muislamu aliye na uwezo wa kugharamikia safari na mahitaji yote.

Ni nguzo ya mwisho katika nguzo tano za Uislamu, na humlazimu Muislamu kusafiri Kwenda hadi mjini Makkah, Saudi Arabia kutekeleza ibada hiyo.

BY NEWS DESK