Mahakama kuu imeamuru kuachiliwa mara moja kwa watu sita, wanaodaiwa kutekwa nyara na maafisa wa wanaodaiwa kuwa maafisa wa serikali.
Akitoa maagizo hayo, Jaji Bahati Mwamuyé pia amezuia kushtakiwa kwao kusubiri matokeo ya kesi kuhusiana na hiyo iliyowasilishwa na Chama cha mawakili (LSK).
Baada ya shinikizo kila pande Mahakama pia imemwagiza Inspekta Jenerali wa Polisi, Douglas Kanja kufika mahakamani binafsi kueleza waliko vijana hao 6.
Kanja, ambaye ni mlalamikiwa wa kwanza katika kesi hiyo, pia ameagizwa kuhakikisha walalamikaji wanafikishwa kortini jinsi alivyoelekezwa ndani ya saa 24.
Uamuzi huo wa mahakama umejiri baada ya ombi la dharura kuwasilishwa na walalamishi hao ambao wamedai kuwa walizuiliwa kinyume cha sheria na polisi na vyombo vingine vya usalama.
Mahakama pia imetoa amri ya kuwazuia polisi na walalamikiwa wengine kuwashtaki au kuwafungulia mashtaka walalamikaji bila idhini ya Mahakama Kuu.
Watu hao sita, ambao ni pamoja na Gideon Kibet (Bull), Barnard Kavuli, na wengine wanne – Peter Muteti, Billy Mwangi, Rony Kiplagat, na Steve Kavingo – wanaripotiwa kuwa waathiriwa wa kutoweka kwa lazima na kuwekwa kizuizini kinyume cha sheria.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama (NTSA), George Njao, au afisa mteule, pia anaamriwa kufika mbele ya mahakama Januari 3, 2025, ili kutoa rekodi mahususi za gari zinazohusiana na kesi.
Haya yanajiri baada ya Seneta wa Busia Okiya Omtatah kuwasilisha kesi Mahakamani kuwashurutisha Wakuu wa Idara za usalama nchini kuwafikisha mahakamani mara moja vijana wote waliotekwa nyara.
Katika kesi yake Omtatah alikuwa amemtaka inspekta mkuu wa Polisi Douglas Kanja, Mkuu wa Idara ya Upelelezi na makosa ya jinai DCI, Mohammed Amin na Mkurugenzi wa Mashtaka ya umma Renson Ingonga kuwafikisha vijana hao mahakamani mara moja.
By Mjomba Rashid