HabariNews

Maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi yapungua kaunti ya Kilifi

Ulimwengu ukiadhimisha siku ya kimataifa ya mipira ya kondomu kila tarehe 13 mwezi Februari, kaunti ya Kilifi kupitia idara ya afya imetangaza kupungua kwa maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi kutoka kwa asilimia 2.8 hadi asilimia 2.5.

Serikali ya kaunti ya Kilifi imesema kwasasa iko na mipira ya kutosha ya kondomu huku ikizidi kusistizia wakazi kutumia mipira hiyo kuendelea kujikinga kila wanaposhiriki ngono.

Kwa mujibu wa Bilal Mazoya msimamizi wa maswala ya afya eneo bunge la Kilifi kaskazini, vijana wanafaa kupewa kipaumbele katika hamasa kuhusu ugonjwa wa ukimwi pamoja na utumizi wa kinga wakati wakushiriki ngono, ili kuendelea kupungua kwa maambukizi hayo kaunti ya Kilifi.

“Mipira ya kondomu iko kwenye program ya NASCOPE ambacho ni kitengo humu nchini kinachosimamia ugonjwa wa ukimwi na magonjwa mengine ya ngono ya kuambukiza. Kwa hiyo kupitia “Global Fund” na wafadhili wengine tunaweza kupata mipira ya kondomu. Kwa hivyo mipira ya kondomu ipo katika vituo vyetu vya afya.” alisema Mazoya.

Dkt. Hamza Bulhan mkurugenzi wa shirika la Aids Healthcare Foundation AHF ukanda wa pwani ameeleza kuwa maambukizi ya virusi vya ukimwi ukanda huu yamepungua, akionya kuwa hamasa na jitihada nyingi zinafaa kulenga kizazi kichanga cha kati ya miaka 15 hadi 35 kwani wao ndio walio kwenye hatari kubwa ya kupata maambukizi.

Ameongeza kuwa shirika la AHF pamoja na wadau wengine wanaendelea kuweka mikakati ili kukabiliana na changamoto ya uhaba utakaoshuhudiwa kufuatia taifa la Marekani kuondoa misaada iliyokuwa ikitoa kwa mataifa mengine.

Vile vile amesema athari hiyo ya kuondolewa kwa misaada kutoka taifa la Marekani hakumaanishi kuwa waathiriwa wa ugonjwa wa ukimwi watakosa dawa za kupunguza makali ya virusi pamoja na huduma nyingine zinazoambatana na ugonjwa huo.

“USAID kuondoka inafaa kutufungua macho kwasababu kama taifa tumekuwa tukitegemea sana wafadhili kama taifa hasa katika maswala ya ugonjwa wa ukimwi. Na tunajuwa imetuchukua miaka mingi mpaka  kufikia tulipo ambapo tunapata huduma hizi bure. Kupima, kupewa dawa za ukimwi kwa hivyo kuondolewa kwa msaada tunajua wazi kwamba kutatutatiza kidogo.

“Viwango vya maambukizi vya sasa ukilinganisha na vile vya mbeleni, sasa hivi viwango hivyo vimepungua.” alisema Bulhani.

Mordecai Odera ofisa wa shirika la Trust for Indigenous Culture And Health TIKA kupitia kampeni mbali mbali za hamasa kwa wananchi, takwimu zinaonesha kuwa kiwango kilichokuwa kikilengwa na serikali  cha asilimia  95 95 95 cha kupima, kuhudumia na kudhibiti watu wanaoishi na virusi vya ukimwi kimeweza kufikiwa.

Odera ameeleza wamepata mafanikio katika jitihada hizo na kufikia asilimia 98 98 94 ya kupima, kuhudumia na kudhibiti ugonjwa huo wa upungufu wa kinga mwili huku akieleza kuwa changamoto inayosalia ni kudhibiti virusi visiongezeke miongoni mwa wangojwa.

Na siku hii ya kimataifa ya kondomu ni njia moja wapo ya kuchangia kufikia kile kiwango cha asilimia 98, 98, 94. Serikali ya kitaifa ilisema lengo lake ni kufikia asilimia 95, 95, 95, ya kupima, kuhudumia na kudhibiti watu wanaoishi na virusi vya ukimwi. Na sisi tumefanikiwa kufikia asilimia 98, 98, 94 ambayo ni mwelekeo mzuri japo changamoto iliyopo ni kuzuia virusi visiongezeke miongoni mwa wagonjwa.” alisema Odera.

Hafla hiyo ya kuadhimisha siku ya kimataifa ya kondomu imefanyika katika chuo kikuu cha pwani mjini Kilifi. Kauli mbiu ya mwaka huu ikiwa ni kujitegemea na kizazi bila ukimwi.

Erickson Kadzeha