Huduma za matibabu katika hospitali za umma kaunti ya Taita Taveta zimeendelea kulemaa kwa zaidi ya wiki 2 sasa kufuatia mgomo wa wahudumu wa afya.
Wahudumu hao wakiwemo maafisa kliniki, wauguzi na wale wa maabara wameendelea kususia kazi na kuapa kutorejea kazini hadi pale Serikali ya Kaunti hiyo itakapotekeleza makubaliano yao ya awali.
Wamefanya maandamano mjini Voi kushinikiza serikali iwalipe mishahara yao iliyocheleweshwa sawia na kuwalipia fedha za bima wanazokatwa.
Wamesema licha ya kaunti hiyo kukosa kutekekeleza hata moja ya makubaliano ya awali, imekuwa ikiwashinikiza warejee kazini jambo wanalosema limewafanya kukosa imani na serikali hiyo.
Sasa wanaitaka serikali hiyo ya kaunti itekeleze makubaliano yao kabla ya kuwashawishi kurejea kwenye mazungumzo ya kurudi kazini.
By News Desk