Huenda ikawa afueni ya muda kwa Wakenya baada ya Mamlaka ya Kudhibiti Kawi na petroli nchini, EPRA kutangaza kupungua kwa bei ya bidhaa za mafuta nchini kwa kipindi cha mwezi mmoja.
Kupungua kwa bei hizo ni kutoka saa sita usiku wa Aprill tarehe 15 hadi Mei 14.
Kwa sasa bei ya petroli imepungua kwa shilingi 1 na senti 95 kwa lita na mafuta ya Diseli nayo yakipungua kwa shilingi 2.20 kwa lita huku mafuta ya taa nayo yakipungua kwa kwa shilingi 2.40 kwa kila lita.
Mjini Mombasa, wenye magari watagharimikia shilingi 171.39, kwa lita moja mafuta aina ya super petrol, na shilingi 161.62 na shilingi 145.75, dizeli na mafuta ya taa mtawalia.
Bei mpya zinazoanza kutekelezwa Aprili 15 zitapelekea lita moja ya super petroli jijini Nairobi kuuzwa kwa shilingi 174.63 jijini, huku dizeli ikiuzwa kwa shilingi 164.86 nayo mafuta ya taa yakigharimu shilingi 148.99 kwa lita moja.
Wakati huo huo, wateja kaunti ya Kisumu watanunua lita moja ya petroli kwa shilingi 174.67, dizeli kwa shilingi 165.24 na mafuta ya taa kwa shilingi 149.42 kwa lita.
Kupungua kwa bei hizi kumetokana na kushuka kwa gharama ya mafuta inayosafirishwa kutoka nje pamoja na mabadiliko ya viwango vya ubadishanaji wa fedha.
By Mjomba Rashid