HabariNews

Bajeti ya fedha za kufadhili zoezi la upanzi wa miti nchini yapitishwa.

Bunge la kitaifa kupitia kamati ya mazingira na misitu limepitisha bajeti ya fedha za kufadhili zoezi la upanzi wa miti nchini.

Mbunge wa Msambweni Feisal Bader ambaye pia ni mwanachama wa kamati hiyo amesema kuwa hatua hiyo itasaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Haya yanajiri huku rais William Ruto akitarajiwa kuzindua rasmi zoezi la kitaifa la upanzi wa miti litakalofanyika katika kaunti zote za humu nchini.

Wakati uo huo, mbunge huyo amewahimiza vijana na wanawake kujisajili kwa makundi ili waweze kufaidika na fedha hizo.

Bader amedokeza kwamba makundi hayo yatatumika kwa shughuli ya upanzi wa miche itakayonunuliwa na serikali.

Huku hayo yakijiri, wakaazi katika maeneo kame ikiwemo Kinango na Samburu kaunti ya Kwale wamehimizwa kuweka kipaumbele upanzi wa miti hususan wakati huu wa mvua chache ili kukabiliana na upungufu wa misitu unaoshuhudiwa maeneo hayo.

Mkurugenzi katika shirika la uhifadhi wa mazingira nchini NEMA tawi la kaunti ya Kwale Godfrey Wafula amesema licha ya wadau mbalimbali kuwekeza katika upanzi wa miti, kuna haja juhudi zaidi kuwekezwa katika upanzi huo wa miti na kuongeza asilimia ya misitu ili kukabiliana na changamoto za kiangazi.

Wafula amezidi kuwahimiza wakaazi kupanda miti zaidi pamoja na kuitunza miti hiyo ili kuboresha mazingira pamoja na kuongeza rutuba katika ardhi kwa minajili ya kilimo.

BY EDITORIAL TEAM